Nyanya shujaa apambana na fisi kichakani na kufaulu kukinga wajukuu wake wadogo wasitafunwe
MWANAMKE wa miaka 54 anauguza majeraha mabaya hospitalini ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu baada ya kushambuliwa na fisi akijaribu kuokoa wajukuu wake wasidhuriwe.
Bi Ebla Abdi, mkazi wa kijiji cha Lake Amu, tarafa ya Mpeketoni, Lamu Magharibi, Jumapili alijipata pabaya pale fisi huyo mla-watu alipong’ang’ana kuwafikia wajukuu wake wawili ili kuwashambulia na kuwala lakini akamdhibiti.
Bi Abdi alikuwa ameondoka nyumbani kwake muda mfupi yapata majira ya saa tano asubuhi na kuelekea kwenye kichaka cha umbali wa mita hamsini hivi kutoka bomani kwake kwa minajili ya kukata fito za kujengea.
Kwa sababu kichaka kilikuwa karibu, Bi Abdi aliandamana na wajukuu wake wawili wadogo ambao ni umri wa miaka minne na sita.
Punde alipoanza kukata fito hizo, ghafla binvuu, fisi alichomoka kutoka kichakani akilenga kuwafikia watoto hao ili kuwadhuru na kupata mlo.
Kwa haraka, Bi Abdi alimrushia fisi huyo upanga aliokuwa ameshikilia mkononi huku akiwaziba wajukuu wake kwa nyuma wasifikiwe na mnyama huyo hatari.
Kutokana na hilo, fisi huyo mwenye njaa alimrukia Bi Abdi na kuanza kumuuma mabegani, mikononi, miguuni na hata usoni.
Kishujaa, mwanamke huyo alianza kupigana na fisi huyo miereka.
Kuona tukio hilo la kutisha, wajukuu hao wawili walipiga mayowe huku wakitorokea nyumbani kwao.
Ni kutokana na purukushani na kelele za watoto hao ambapo majirani walijitokeza kwa wingi wakiwa wamejihami kwa visu, mapanga na marungu.
Walifika eneo la tukio ambapo walimzingira fisi, wakamwandama na kumpiga hadi kufa.
Wakati huo, tayari Bi Abdi alikuwa ameanguka upande mmoja akivuja damu mikononi, miguuni, kifuani, sehemu ya mbavu na usoni.
Majirani walimchukua mwanamke huyo na kumkimbiza kwenye hospitali ya Mpeketoni alikolazwa kwa matibabu.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, mumewe mhasiriwa, Bw Abdi Saweni Barisa, alishukuru Mungu na majirani kwa kusaidia kukabiliana na fisi na kuokoa maisha ya mkewe yaliyokuwa hatarini.
Bw Barisa alilitaja tukio hilo kuwa la kutisha na la kuumiza, ambapo aliomba serikali kupitia Shirika la Huduma kwa Wanyama Pori nchini (KWS) kuifidia familia yake.
“Mke wangu ameachwa na majeraha mabaya karibu kila mahali kwenye mwili wake. Amelazwa hapa hospitalini Mpeketoni. Sisi wenyewe ni maskini. Hata hatujui bili ya matibabu tutailipaje. KWS wafikirie kumfidia mke wangu kwa majeraha aliyosababishiwa na fisi huyo,” akasema Bw Barisa.
Mwanaharakati wa kijamii Lamu, Bw Kimani Wanyoike Kimwa alikashifu vikali KWS kwa kuzembea katika kuwadhibiti wanyama pori wasifikie makazi ya binadamu.
Bw Kimwa aliishinikiza KWS kuhakikisha Bi Abdi na wengine wengi ambao wamejeruhiwa, kuuliwa au mimea yao kuharibiwa na wanyama pori Lamu wanafidiwa mara moja.
“Kila mara watu wetu hapa Mpeketoni na Lamu wamejitokeza kuomba KWS wadhibiti wanyama wao. Utapata fisi, mayonda, nyati na hata simba wakivamia maboma ya watu wakitafuta chakula na maji. Kuna visa vya watu kuuawa au kujeruhiwa, mifugo, ikiwemo mbuzi, kondoo na punda kung’atwa na hata kuuawa. Baadhi ya visa hivyo havijafidiwa. Ni wajibu wa KWS kuhakikisha hivyo visa vinavidiwa na wanyama pori wadhibitiwe vilivyo,” akasema Bw Kimwa.
Katika mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu Jumatatu, Naibu Mkurugenzi wa KWS Kaunti ya Lamu, Bw Ibrahim Ahmed alithibitisha kisa cha mwanamke huyo kushambuliwa na kujeruhiwa na fisi kijijini Lake Amu.
Bw Ahmed alisema kisa hicho kinafuatiliwa kwa karibu kwani tayari maafisa wa KWS walitumwa eneo hilo kutathmini hali na kuandika ripoti yao.
Aliisihi familia ya Bi Abdi na waathiriwa wengine kuhakikisha wanaripoti haraka hasara wanayokadiria, ikiwemo vifo na majeruhi yanayosababishwa na wanyama pori punde yanapotokea maeneo yao.
“Tumewaelekeza wanafamilia ni nini cha kufanya ili kuwasaidia watume fomu za kuomba fidia Nairobi mara moja. Visa vya migogoro ya wanyama pori na binadamu vikiripotiwa mapema vitashughulikiwa kwa haraka. Wananchi pia waepuke kubuni makao na mashamba kwenye maeneo ambayo ni njia au makazi ya wanyama,” akasema Bw Ahmed.