Makala

Nyoro aonekana mpweke kisiasa akishukiwa kuwa mradi

Na  Mwangi Muiruri August 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Kati ya wanasiasa wakuu wa eneo la Mlima Kenya waliopigwa darubini kisiasa baada ya Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kuondolewa madarakani mwezi Oktoba 2024, ni Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro.

Nyota ya kisiasa ya Nyoro iling’aa baada ya Rais William Ruto kuapishwa mnamo Septemba 13, 2022, huku baadhi ya wafuasi wake wakimpigia debe kuwa ndiye mrithi bora wa uongozi  eneo la Mlima Kenya  hata kabla ya sakata ya kumuondoa Gachagua kuanza.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu aliwahi kumsihi Rais Ruto kumchagua Nyoro kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa 2027, akidai Gachagua hakuwa na uwezo wa kuunganisha eneo la Mlima Kenya wala kumsaidia Rais kupata muhula wa pili.
“Ukiwa na Gachagua kama mgombea mwenza 2027, utapata shida. Kwa wengi wetu, mtu pekee anayeweza kuunganisha Mlima Kenya na kukusaidia kushinda ni Nyoro,” Nyutu alinukuliwa akisema wakati huo  ingawa kwa sasa ni mmoja wa wafuasi wa karibu wa Gachagua.

Hata hivyo, Nyoro alichukua msimamo wa kimya wakati wa mchakato wa kuondolewa kwa Gachagua bungeni, na sasa anaonekana kana kwamba ni mpweke kisiasa hana mwelekeo bayana wa kisiasa, wala hajiungi na kambi yoyote.

Tofauti na upande wa upinzani unaoongozwa na Gachagua unaoandaa mikutano ya pamoja na mikutano ya wanahabari, Nyoro anaonekana kuendesha siasa peke yake. Amekuwa akitoa taarifa za kiuchumi kuhusu bajeti ya mwaka wa 2025/2026, madeni ya kitaifa, bei ya mafuta, na mipango ya barabara za kulipia ushuru  akizungumza akiwa peke yake mbele ya waandishi wa habari.

Kufuatia msimamo wake wa kukosoa serikali ya Ruto, Nyoro aliondolewa kwenye Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Fedha na kuhamishwa hadi Kamati ya Wakenya wanaoishi ng’ambo isiyo na ushawishi mkubwa.

Awali, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti lakini nafasi hiyo ilichukuliwa na Mbunge wa Alego Usonga kutoka ODM, Samuel Atandi  mshirika wa karibu wa Raila Odinga. Hii ilitokea wakati wa mabadiliko makubwa ya uongozi bungeni yaliyowanufaisha wabunge wa Kenya Kwanza waaminifu kwa rais na washirika wa ODM.

Kwa sasa, kambi ya Gachagua inamtazama Nyoro ikimtaka ajiunge nao au aeleze bayana msimamo wake, la sivyo atachukuliwa kama “mradi” wa kugawanya kura za Mlima Kenya.

Katika mahojiano ya runinga ya Inooro TV, Gachagua alimwambia Nyoro:“Tangaza msimamo wako kuhusu maslahi ya Mlima Kenya. Kimya chako hakisaidii. Tunataka kujua hesabu yetu ni ipi. Mambo ya jamii si ya watu wa kunyamaza.”

Kiongozi wa vijana wa chama cha Democratic Congress, Bi Gladys Njoroge, alisema kuwa eneo la Mlima Kenya kwa sasa linayumbishwa na makundi matatu makuu: la Rais Ruto, la Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, na la Gachagua. “Ndindi Nyoro kwa sasa anatembea katikati ya makundi haya,” alisema.

Bi Njoroge aliongeza kuwa chama kipya cha Democracy for Citizens Party (DCP) kilichoasisiwa na Gachagua na muungano wake wa upinzani dhidi ya Ruto tayari kimevutia hisia za wakazi wa Mlima Kenya.
“Wakati wote, Nyoro lazima ajue kuwa uwanja wa Mlima Kenya ni mgumu,” akaonya. “Tumewaona wanasiasa waliokuwa maarufu kama Martha Karua, Peter Kenneth, Wangari Maathai wakiadhibiwa kwa kupinga msimamo wa jamii.”

Katika miezi miwili iliyopita, Nyoro amekuwa akizungumza zaidi kuhusu masuala ya kiuchumi, ujenzi wa barabara, mgao wa fedha kwa shule, deni la kitaifa, na mauaji ya kiholela. Lakini katika taarifa zake, huwa hatamki majina ya Rais Ruto, Gachagua, Odinga au Kenyatta  labda kwa makusudi ya kujenga sura ya kiongozi huru anayejitegemea kisiasa.

Wapo wanaoamini kuwa Nyoro alikuwa ameweka matumaini ya kunufaika na kuporomoka kisiasa kwa Gachagua na kuwa kiongozi wa Mlima Kenya. Lakini hali imebadilika.

Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango alisema:“Waliopanga njama ya kumuondoa Gachagua walitarajia angesahaulika haraka kama aliyekuwa Makamu wa Rais wa tano Josephat Karanja (1988/1989). Lakini Gachagua amevuka matarajio na kuwa mwenye ushawishi mkubwa zaidi.”

Kimya cha Nyoro wakati wa hatua ya kumuondoa Gachagua hakikupita bila kukosolewa. Baadhi ya washirika wa Ruto kutoka Mlima Kenya, akiwemo Naibu Rais mpya Prof Kithure Kindiki, walimkosoa hadharani, wakidai hana ushawishi mkubwa.

Hata hivyo, mnamo Aprili 1, 2025, Rais Ruto alisema katika mkutano na wanahabari katika Ikulu ndogo ya Sagana:“Nyoro ni mtu ninayefanya naye kazi. Namlea kisiasa na naona ana matumaini makubwa ya uongozi.”