Makala

Nyota wa ulinzi Amboseli

August 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

HUKU ulimwengu ukiendelea kupambana na athari zinazotokana na mkurupuko wa maradhi ya Covid-19, sekta ya utalii ni mojawapo ya nyanja zilizoathirika pakubwa.

Kwa upande mwingine, upungufu wa mapato kutokana na utalii, umekuwa tishio kwa sekta zingine, kama vile ile ya uhifadhi wa wanyamapori.

Lakini licha ya changamoto hii, kuna hadithi za matumaini na mojawapo yazo ni ile ya walinzi wa kike wa hifadhi ya wanyamapori ya Amboseli, ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha usalama wa wanyama na jamii.

Bi Eunice Mantei, ni mmoja wa wanawake hao wachache kati ya umri wa miaka 20 na 30 wanaohudumu kama walinzi katika mbuga hii huku wakikumbwa na jukumu la kuwalinda wanyamapori kutokana na majangili, vile vile kuwalinda watu wanaoishi katika eneo linalozingira mbuga hii.

Bi Mantei alijiunga na kundi hili Machi 1, 2019, miezi michache tu baada ya kukamilisha masomo ya shule ya upili.

Kwa upande wake Bi Purity Amleset Lakara, 23 alianza kazi hii, pia pindi baada ya kukamilisha shule ya sekondari.

Lakini mwanzoni haikuwa rahisi kwake kwani alilazimika kupambana na dhana na itikadi za kijamii.

“Kawa kawaida, kulingana na jamii ya Wamaasai, wanawake hawakutarajiwa kufanya kazi za aina hii kwani walionekana kuwa dhaifu. Lakini muda ulivyozidi kusonga, dhana hii ilibadilika na sasa tunakubalika,” aeleza Bi Lakara.

Mojawapo ya vichocheo vilivyowasukuma katika nyanja hii ilikuwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa wanyamapori katika jamii. Wawili hawa wanasema kwamba waliamini kwamba, hii ingesaidia kutatua tatizo la mgongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Kama walinzi wengine, kazi yao inahusisha kufuatilia wanyama kukagua iwapo kuna lishe ya kutosha, vile vile kupiga doria mwituni kuhakikisha kwamba wanyamapori wako katika afya njema, na ikiwa sivyo, kutoa taarifa.

Bi Eunice Mantei (kushoto) na Bi Purity Lakara (kulia). Picha/ Hisani

“Aidha tunapiga doria kuhakikisha kwamba hakuna uharibifu wa mimea katika hifadhi hii. Hii inaafikiwa kwa kuingiliana na jamii ili kupata taarifa na maoni ambayo yatanufaisha wanyamapori, vile vile jamii,” aeleza Bi Mantei.

Kwa kawaida, Bi Mantei anasema kwamba wao hukumbana na changamoto ikiwa ni pamoja na kushambuliwa na wanyamapori kama vile nyati, ndovu.

Kwa upande wake Bi Lakara anasema kwamba kuna wakati ambapo wanakumbwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kazi, suala ambalo limekuwa likiathiri kazi zao.

Lakini licha ya changamoto hizi, jitihda zao zimeimarisha hali ya mbuga hii. Mwaka jana, shirika la huduma ya kitaifa ya uhifadhi wa wanyamapori KWS ilitangaza kupungua kwa visa vya uwindaji haramu. Takwimu za shirika hili zilionyesha idadi ya ndovu waliouawa na majangili mwaka wa 2018, ilikuwa 38 ikilinganishwa na 384 mwaka wa 2012. Kwa upande mwingine, idadi ya vifaru waliouawa kwa sababu ya pembe ilipungua kutoka 30 hadi wanne.

Mbali na hayo, msimu huu wa mkurupuko wa maradhi ya Covid-19 unaendelea kuwa tishio kwa mafanikio haya.

“Maradhi haya yamebadilisha ratiba yetu ya kazi yetu kwani kwa sasa hatupati wiki moja ya mapumziko kama ilivyokuwa awali, suala ambalo limeathiri muda wetu na familia zetu,” asema Bi Lakara.

Aidha, ratiba yao ya kupiga doria imebadilika kutokana na hofu ya ongezeko la visa vya uwindaji haramu.

Lakini licha ya changamoto hizi, wana matumaini mengi ya siku zijazo, huku wakiendelea kufurahia kazi ambayo kwa muda mrefu haikutarajiwa kufanywa na wanawake.