Nyota wa zamani wa Harambee Stars anavyohangaika akichoma makaa
GABRIEL KUDAKA NA LABAAN SHABAAN
MILIO ya shoka likigonga visiki vya miti inasikika katika maeneo tulivu ya Kimalel, Eldoret huku Patrick Namai aking’ang’ana kupasua magogo ya miti kuwa vipande vidogo vya kuchoma makaa.
Mara kwa mara anasitisha ukataji kupangusa jasho lisitiririke machoni kabla ya kuendelea na kazi.
“Hiki ni kisiki cha tatu cha mti ninachokata. Nimemaliza kung’oa visiki viwili na kuvikata vipande ambavyo vinakauka pale,” Bw Namai anasema anapotukaribisha katika siku ya kawaida ya maisha yake ya sasa.
Beki huyo wa zamani wa Harambee Stars aliwahi kucheza na wachezaji mashuhuri wa kulipwa.
Aliaga soka miaka 30 iliyopita na tangu wakati huo amekuwa akitapatapa kujikimu kimaisha mjini Eldoret.
Alisakata gozi na wachezaji wa kulipwa kama Paulo Maldini, nguli wa soka wa Italia ambaye alichezea klabu tofauti kama vile AC Milan.
“Nilipokuwa Italia nilicheza na wachezaji stadi kama Paulo Maldini. Alinipa jezi baada ya mchuano kwa sababu alipenda jinsi nilivyocheza. Nilikuwa difenda wa katikati,” alisema.
Bw Namai, anahangaikia maisha akichoma makaa katika eneo la Langas, Kaunti ya Uasin Gishu.
“Sio maisha rahisi. Hata haya mashina ninayong’oa ili kutengeneza makaa si yangu. Kuna mtu amenipa kazi. Siwezi tu kukaa tu. Nina familia ya kutunza na ndiyo maana ninafanya kila aina ya kazi za kawaida,” anaeleza.
Alizaliwa mwaka wa 1966 katika mtaa wa Makongeni, Nairobi. Usogora wa kandanda wa Namai uliboreshwa akiwa katika Shule ya Msingi ya Union, Eldoret.
Hii ilikuwa baada ya babake, marehemu Naftali Gadi Namai, kuhamishwa hadi Eldoret akiwa mfanyakazi wa Shirika la Reli la Kenya.
“Nilianza kupendezwa na soka nikiwa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi ya Union. Nilichezea timu ya shule hadi ngazi ya kitaifa,” aliambia Taifa Leo.
Baadaye alijiunga na Shule ya Msingi ya Kapsoya, ambako alifanya mtihani wa kitaifa mwaka wa 1983 na kupata alama 32 kati ya 36.
Alama hizi zilimwezesha kusajiliwa katika Shule ya Upili ya Kakamega kati ya 1983 na 1989.
Kipaji chake kilikuzwa zaidi na aliyekuwa mkufunzi wa soka wakati huo marehemu Chris Makokha alipokuwa akibukua vitabu katika Shule ya Upili ya Kakamega.
Bw Patrick aliichezea timu ya Taifa ya Chipukizi chini ya umri wa miaka 21 katika miaka ya 80.
Alikuwa katika kikosi cha timu ya taifa iliyocheza nchini Italia na Zambia mwaka wa 1986 na 1987 mtawalia.
“Sikumbuki jina la mashindano hayo, lakini Kenya ilicheza dhidi ya mataifa mengine. Haikuwa mechi ya kirafiki,” alisema.
Anakumbuka goli alilofunga akiwa nahodha kwa njia ya penalti iliyoipatia timu yake ushindi nchini Zambia.
“Kocha wangu Chris Makokha wakati huo alikuwa kipofu, lakini alisherehekea ushindi huo. Mike Okoth ambaye sasa anaselelea Ubelgiji alikuwa mlindalango wetu wakati huo,” alisema Namai huku akicheka.
Baada ya sare ya bila mabao, katika fainali hizo, Kenya ilifunga mabao 5-4 dhidi ya Zambia kwenye mechi iliyogaragazwa katika uwanja wa Nkana mjini Kitwe nchini Zambia.
Bw Namai ambaye alikuwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya chipukizi chini ya umri wa miaka 21 iliyowakilisha Kenya anaarifu Kenya ilishindwa na Italia 1-2.
Kwa miaka sita ambayo Namai alichezea Shule ya Upili ya Kakamega, walishinda fainali zote isipokuwa 1985 wakati timu yake iliposhindwa na Shule ya Upili ya Musingu.
“Musingu walitushinda 2-1 katika mchezo huo uwanjani Bukhungu, Kakamega,” alikumbuka.
Tangu 1986, Bw Namai amehifadhi jezi hiyo kama kumbukumbu na huvaa katika hafla maalum.
Licha ya kupata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno baada ya kisomo cha sekondari, Bw Namai aliamua kuchezea Rivatex FC Eldoret.
Hapa alifanya kazi katika idara ya uhasibu. Baada ya muda mfupi akiwa Rivatex, alihamia Kenya Cooperative Creameries (KCC) Eldoret ambako alifanya kazi kando na kucheza kati ya 1992 hadi 1998 hadi KCC ikasambaratika.
“Mnamo 1994, timu yangu, KCC ilishinda AFC Leopards 3-1 wakati wa Moi Golden Cup,” anakumbuka Namai.
Akiwa KCC, Namai alicheza pamoja nao Peter Kihamba, Tom Arero, Ken Abundo, na Mark Sirengo, miongoni mwa wengine. Baadaye alistaafu mwaka wa 1996.
Anaeleza kocha wake wa KCC alimwomba achague kati ya kazi na soka aliporejea kutoka Mombasa alipoenda kwa shughuli za kazi kwa wiki moja.
“Nilichagua kazi. Hilo ndilo lililonifanya niache soka,” alisema.
Bw Namai anadokeza kuwa enzi hizo, soka haikuwa na malipo mazuri kama ilivyo sasa. Wengi wao walitumia soka kama njia ya kupata ajira katika kampuni kama vile Mumias Sugar Company, Rivatex, Kenya Cooperative Creameries, Kenya Breweries, na Kenya Ports Authority.
“Lengo langu lilikuwa kuajiriwa kwa mkataba wa kazi ya kudumu KCC lakini hilo lilikatizwa wakati kampuni ilipoanguka,” anaongeza Namai.
Anafichua kuwa mafanikio pekee aliyopata kutokana na soka ni kuajiriwa KCC.
Bw Namai alichezea timu ya taifa kwa miaka miwili (1992 na 1993) ambapo alicheza pamoja na majina mengine mashuhuri kama vile Musa Otieno, Mike Wambani, Francis Oduor, na Sammy “Pamzo” Omollo.
Baba huyo wa watoto sita anakosoa Shirikisho la zamani la Soka Kenya akidai liliendesha kandanda vibaya na kukosa kuunga mkono wachezaji.
“Serikali inapaswa kuweka mifumo ya kusaidia wachezaji mashuhuri. Nikitumia mfano wa riadha, wanariadha wengi wa Kenya wamekwenda nchi jirani kama vile Uganda kwa sababu wanatunzwa vizuri huko. Kwa hivyo wachezaji wazuri wanafaa kupigwa jeki,” anaongeza Namai.
Licha ya kufana katika kandanda, wakazi wenzake ambao ni wateja wake hawana hata habari kuwa aliwahi kuwa mchezaji wa hadhi kubwa.
Mzee wa Kijiji Hassan Mungare hajui kama Bw Namai alikuwa jina tajika.
“Huyu mtu ninamfahamu kama mchomaji makaa. Sijawahi kujua kuwa alikuwa mtu maarufu kiasi hiki aliyeiletea nchi fahari,” alisema Bw Mungare.
Namai anatumai kuanzisha mpango tofauti wa kumtegea uchumi iwapo atapata Msamaria Mwema.
Shabiki huyo wa Manchester United anawasihi wazazi kuunga mkono vipaji vya watoto wao.