Makala

OBARA: Tusidanganyane, Kenya haitapata mageuzi punde

February 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Kinara wa muungano wa NASA na mwenyekiti wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

WIKI iliyopita, Wakenya wanaotamani mageuzi ya kuongoza taifa hili walijawa na matumaini upya kwamba huenda mageuzi hayo yakapatikana hivi karibuni.

Hii ilitokana na jinsi aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Bw Jacob Zuma, alivyojiuzulu mamlakani kisha saa kadhaa baadaye Waziri Mkuu wa Ethiopia, Bw Hailemariam Desalegn, akajiuzulu.

Wakenya ambao hawaridhishwi na mienendo ya utawala uliopo walijitia moyo kwamba kuna wimbi la mageuzi linalovuma Afrika, hasa ikizingatiwa jinsi aliyekuwa rais wa Zimbabwe, Bw Robert Mugabe alivyong’atuliwa mamlakani mwishoni mwa mwaka uliopita.

Nami ningependa kuwavunja moyo wananchi hao wazalendo na kuwaomba wakome kujipumbaza, kwani humu nchini hatujapata wakombozi wenye ari kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi yatakayowafaa wananchi wa kawaida.

Kufikia sasa, tegemeo pekee la wananchi aina hii liko kwa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ingawa akiwa peke yake hawezi kufanikisha maazimio hayo.

Si siri kwamba hali inayoshuhudiwa humu nchini haina tofauti kubwa na jinsi hali ilivyokuwa katika enzi za utawala wa chama kimoja.

Ishara zake ni ukandamizaji wa haki za wakosoaji wa serikali, uhuru wa vyombo vya habari kupigwa breki, serikali kuu kudharau mamlaka ya mahakama na kukandamizwa kwa mashirika ya kutetea haki za kijamii.

Serikali iliyopo ilianza kwa kukandamiza mashirika ya kutetea haki za kijamii ambazo hivi sasa hazisikiki. Baadaye mahakama ilitekwa kupitia kwa vitisho na hivi sasa kuna ishara za kuiteka hata zaidi. Tuliona vyombo vya habari vikifyatwa na uhuru wao ukavyogwa.

Wakati wa mapambano ya kupigania siasa ya vyama vingi, asasi hizi zote zilishirikiana bila kujali maslahi yao ya kibinafsi kwani lengo kuu lilikuwa kuikomboa taifa kutoka kwa minyororo ya utawala wa kiimla.

 

 

Ubinafsi

Tofauti na enzi hizo, kwa sasa tunashuhudia hali ambapo viongozi wa kisiasa ambao wangemtia nguvu Bw Odinga katika juhudi zake wamejaa ubinafsi mkubwa.

Sisemi eti Kinara huyo wa NASA hana maazimio yake ya kibinafsi, bali ana rekodi iliyo wazi kuhusu alivyowahi kujitolea mhanga ili kutetea wananchi.

Vinara wenzake ambao wangemsaidia wamedhihirisha kuwa ni waoga, na sasa macho yao yamelenga uchaguzi wa 2022 licha ya kudai uchaguzi uliopita haukufanywa kwa njia ya haki. Huu ni undumakuwili wa hali ya juu!

Bungeni nako wabunge wa upinzani hawajifahamu kama wanataka kutetea haki za wananchi au kujilimbikizia mali.

Tegemeo la wanaotamani mageuzi limebaki mikononi mwa wananchi wenyewe, lakini wao pia wametekwa na mgawanyiko wa kikabila unaowafanya kufuata kikondoo viongozi walio serikalini na katika upinzani bila kuwaza kwa makini.

Hivyo basi ni heri sote tukae kitako tusubiri uchaguzi mwingine 2022.