OBARA: Tuwazie upya utunzaji mazingira na ugavi wa ardhi
Na VALENTINE OBARA
UAMUZI wa serikali kutimua watu kutoka Msitu wa Mau na sehemu nyingine zilizolindwa ili kutunza mazingira unazidi kuibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi na viongozi wa kisiasa.
Hii si mara ya kwanza hali hii kutokea na bila shaka, sitarajii itakuwa mara ya mwisho.
Kando na janga la unyakuzi wa ardhi za umma ambalo ni donda sugu hapa Kenya, hali hii huchangiwa pia na jinsi idadi ya watu inavyozidi kuongezeka kimataifa.
Idadi ya watu inapoongezeka, sehemu za ardhi zinazoweza kutumiwa kwa makazi, kilimo na ufugaji ni zile zile. Haziwezi kuongezeka.?Hakika, vipande vikubwa ikiwemo vinavyonyakuliwa kutoka kwa umma vimo mikononi mwa mabwanyenye ambao hawajali kuhusu raia wa kawaida.
Mtafaruku kuhusu umiliki wa ardhi kwa masikini katika jamii huwa hautokei tu kati yao na serikali bali pia kati yao na matajiri wanaomiliki sehemu kubwakubwa za ardhi.
Vilevile, migogoro hutokea kati yao wenyewe kwa wenyewe hasa inapokuwa kwamba upande mmoja kuna wakulima wa mimea na upande mwingine wafugaji.
Haya yote yanaweza kupata suluhisho la kudumu ikiwa tu, viongozi wetu watatumia busara ya kuhusisha wataalamu wa masuala ya utunzaji mazingira, usimamizi wa ardhi na wa mipangilio ya maendeleo ili kuwe na sera maalumu za kugawia wananchi ardhi wanazohitaji.
Mbinu moja ambayo inaweza kusaidia kusuluhisha tatizo la migogoro ya ardhi ni kuweka sera na sheria ambazo zitaruhusu umma kutumia maeneo yanayolindwa kimazingira, huku wakijitolea kuyahifadhi.
Hii ni mbinu ambayo tayari hutumiwa kwa jamii chache zinazoruhusiwa kuishi misituni. Changamoto huwa ni wakati wananchi hao wanapoanza kuharibu rasilimali zilizopo katika maeneo hayo kwa mfano kuanza kukata miti misituni kwa uchomaji makaa.
Changamoto kama hii inaweza kutatuliwa kwa kuwapa wananchi hao mbinu za kujikimu kimaisha wanapokuwa humo misituni.?Kuna miradi inayoendelezwa na mashirika ya kibinafsi ambapo umma hufunzwa jinsi ya kuvuna matawi ya miti yanayotumiwa kutengeneza makaa badala ya kukata mti mzima, na huhamasishwa kuzidi kupanda miti.
Miti wanayopanda ni ile inayoweza kutegemewa kwa ufugaji nyuki na mengine huzalisha vitu muhimu vinavyoweza kutumiwa kiriziki bila kuharibu msitu, kama vile dawa za kienyeji na gundi.
Kwa sasa tunaweza kuvutana kwa maneno kila mara serikali inapoamua kufurusha watu kutoka maeneo yaliyolindwa huku kila mmoja wetu akitaka kuonyesha ugwiji wake wa masuala ya utunzaji mazingira au utetezi wa haki za binadamu.
Lakini tukumbuke, idadi ya watu imetabiriwa kuzidi kuongezeka na ni muhimu tutafakari njia maalumu za kutengea wananchi ardhi hata tunapolinda mazingira yetu.