OBARA: Ulafi uwekwe kando katika marekebisho ya katiba
Na VALENTINE OBARA
KWANZA pongezi kwa Chama cha Thirdway Alliance kwa hatua iliyopiga katika juhudi za kurekebisha katiba.
Mafanikio ya kuruhusiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendeleza mbele juhudi hizo baada ya kukusanya saini halali za wapigakura zaidi ya milioni moja, ni hatua kubwa.
Ijapokuwa kuna tetesi kwamba huenda mikono fiche iliyo na ushawishi katika utawala wa nchi ilihusika kufanikisha mchakato huo kufika ulipo sasa, pongezi ni kwa Dkt Ekuru Aukot na kikosi chake kwani wao ndio walikuwa katika mstari wa mbele machoni mwa umma.
Si siri kuwa wananchi wengi wanatamani sana marekebisho ya katiba hasa ikizingatiwa gharama ya kulipa viongozi wa kisiasa.
Katiba ya 2010 iliongeza idadi ya viongozi ilhali wengi wao hawajali masilahi ya umma.
Uongozi serikalini umegeuzwa kuwa nafasi ya walafi kujitafutia utajiri kwa haraka wakitumia vibaya mamlaka waliyopewa kuwakilisha umma, na vilevile wakipora mali za umma bila huruma.
Ni kwa msingi huu ambapo wengi wetu tungependa kupewa uhuru wa kuamua upya kama kweli tunahitaji kuendelea kuwa na nafasi nyingi za uwakilishi wa kisiasa, ambazo hazisaidii kivyovyote kuboresha maisha yetu.
Kwa mtazamo wangu, huenda ikawa vigumu kushawishi madiwani kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba kwani mamlaka yao ni miongoni mwa yale yanayolengwa kufanyiwa mabadiliko.
Wakati huu tayari tumeanza kusikia wabunge wawakikishi wa kike katika kaunti wakipinga mapendekezo ya kurekebisha katiba kwani nafasi hiyo pia imelengwa kuondolewa.
Huu ni wakati ambapo wanasiasa wanapaswa kutathmini mapendekezo hayo kwa kina na kuona manufaa yake kwa taifa zima badala ya kuendelea kujijali wao wenyewe.
Lakini kutarajia hili itakuwa ni sawa na kuotea embe chini ya mnazi.?Kinachotia moyo ni kuwa Wakenya wengi huonyesha wamechoshwa na jinsi wanasiasa wanavyozidi kuwa walafi kila kukicha, na hivyo basi naamini haitakuwa rahisi kwao kushawishiwa kwamba nafasi nyingi za uongozi wa kisiasa zinafaa ziendelee kuwepo.
Wanasiasa wachanuke, wajue wengi wao wamechosha wananchi kwa uzembe na ulafi wa kupindukia.?Endapo viongozi watakataa kupitisha mswada wa kurekebisha katiba ili uidhinishwe na Rais Uhuru Kenyatta, basi tuko tayari kuwaonyesha kivumbi kwenye debe wakati mswada huo utakapoletwa kwetu tujiamulie kupitia kwa kura ya maamuzi.
Hakika, utamu wa katiba yetu ni jinsi ilivyoachia raia wa kawaida nafasi kujiamulia kuhusu suala zito kama hili.