• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
OCS aomba kupewa kichwa cha mshale uliomdunga kukihifadhi  

OCS aomba kupewa kichwa cha mshale uliomdunga kukihifadhi  

NA MWANGI MUIRURI 

KAMANDA wa Polisi Kituo cha Juja, OCS, John Misoi aliyedungwa kwa mshale wakati akiongoza maafisa wake kuendesha oparesheni dhidi ya wagema wa chang’aa na wauzaji bangi, sasa anaomba kupewa kipande cha kichwa cha mshale kilichotolewa kwenye goti lake ili akihifadhi kama kumbukumbu.

Hii ni baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Avenue iliyoko Mjini Thika na kikatolewa.

Alikumbana na janga hilo usiku wa kuamkia Aprili 1, 2024 katika Kijiji cha Gachororo, Kaunti ya Kiambu alipoongoza kikosi cha uvamizi katika danguro moja.

Bw Misoi alikuwa ameshika doria nje ya danguro hilo huku wenzake wakiwa ndani wakipekua wakati alilengwa kwa mshale kutoka gizani.

Alikimbizwa hospitalini akiwa amezimia na baada ya ‘kufufuliwa’, akafanyiwa upasuaji uliotoa kipande cha kilichochongwa.

Alidungwa kwenye goti.

Ripoti ya madaktari wa Avenue Hospital ilisema kwamba mshale huo ulipenya sentimita tatu ndani ya goti lake la kulia na kuharibu mishipa na pia kuvunja mfupa.

Bw Misoi alisema kwamba uchungu na mshtuko uliomkumba baada ya kushambuliwa na pia taharuki ya mauti angependa kuweka kipande hicho cha mshale kama ushahidi kwake nyumbani.

“Ni vyema kujiwekea ushahidi wa masaibu haya kwangu nyumbani, ili uwe kama motisha kwa hata watoto wangu jinsi baba yao alijituma kudumisha usalama wa nchi kwa manufaa yao na vizazi vijavyo,” akasema.

Aidha, alisema shambulizi hilo ni hamasisho kwake na maafisa walio chini yake kwamba “kazi ya polisi ni huduma kwa binadamu”.

Naibu wa Rais Bw Rigathi Gachagua alimtembelea hospitalini na kando na kumpa ufadhili wa kifedha, akamuahidi mema zaidi kazini kwa tendo lake la kishujaa.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kiambu, Bw Michael Muchiri pia alimtembelea Bw Misoi hospitalini na akampa pole za Inspekta Mkuu wa polisi Bw Japhet Koome.
Alisisitiza kwamba shambulizi hilo halitalemaza juhudi kuhakikisha Kijiji cha Gachororo kimetiwa adabu ya kutii kukoma upishi na uuzaji wa pombe haramu, pamoja ulanguzi wa mihadarati.

Bw Muchiri aliongeza kwamba maafisa wa ujasusi na wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCIO) walitumwa eneo hilo kunasa waliotekeleza shambulizi hilo na tayari wawili wametiwa nguvuni na kushtakiwa.

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Watawa walalamikia visa vya wakongwe kutelekezwa jamaa zao...

LuLu Hassan akiri kuangukia mume wa kishua, Rashid Abdallah...

T L