• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
ODONGO: BBI: Viongozi wa kidini wana kibarua kigumu

ODONGO: BBI: Viongozi wa kidini wana kibarua kigumu

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa kidini kwa mara nyingine wamejitokeza kupinga kupitishwa kwa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) jinsi ilivyo sasa bila kufanyiwa marekebisho zaidi.

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB) wiki iliyopita lilitoa taarifa ya kukosoa baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti hiyo na likaapa kuipinga iwapo itapigiwa kura ya maoni jinsi ilivyo.

Kati ya masuala waliyoyasema yanazua utata ni Rais kupewa mamlaka makubwa ya kuwateua Waziri Mkuu na Manaibu wake wawili, kuongezwa kwa idadi ya maseneta hadi 94 pamoja na idadi ya wabunge kuwa 360.

Pia walisisitiza kuwa ripoti hiyo inampa Rais mamlaka zaidi jinsi ilivyokuwa enzi za utawala wa chama kimoja na kabla ya kupitishwa kwa katiba mpya ya 2010.

Kando na maaskofu wa kanisa katoliki, viongozi wa dini mbalimbali pia wamejitokeza kusema ripoti ifanyiwe mabadiliko.

Kwanza, hoja zilizoibuliwa na viongozi hao wa makanisa zina mashiko lakini ni dhahiri kuwa kilio chao hakiwezi kusikika na kuzingatiwa na wanasiasa.

Kinara wa ODM Raila Odinga tayari amethibitisha kuwa hakuna nafasi ya ripoti kufanyiwa marekebisho zaidi na hafla ya uzinduzi wa kukusanya saini milioni moja itazinduliwa wiki hii.

Je, hayo marekebisho wanayoyapigania viongozi wa makanisa yatafanyika vipi ilhali Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatt hawaonekani kumakinikia suala hilo?

Pili, viongozi wa makanisa hawana ufuasi kutoka kwa wapigakura ikilinganishwa na wanasiasa wakuu nchini ambao hushabikiwa sana na makabila yao.

Ni dhahiri kwamba hata maaskofu wakipinga BBI mwishowe, uwezekano wa kupata ushindi ni finyu mno kwa kuwa waumini wao hufuata kauli za wanasiasa kuliko zao.

Katika kura ya maamuzi 2010, viongozi wa makanisa walipiga kampeni kali ya kupinga katiba ya sasa. Hata walidai inaruhusu uavyaji mimba lakini mwishowe walishindwa kuwashawishi waumini wao kuikataa debeni.

Kushindwa huko pia kunawakodolea macho kwa mara nyingine kwa kuwa BBI imetekwa na wanasiasa ambao nia yao kuu ni kuhakikisha maslahi yao yanatimia.

Hata hivyo, viongozi wa kidini wanafaa wajilaumu wenyewe kwa misimamo yao kutochukuliwa kwa uzito kuhusiana na masuala mbalimbali ya kitaifa.

Wakati wa ghasia za uchaguzi 2007 na 2017, wakuu hao wa kidini walishtumiwa kwa kutochukua hatua uvunjaji wa haki za kibinadamu na mauaji yakiendelea.

Huenda ni vigumu kwao kuwakaripia wanasiasa ambao huwapa hisani kwa hushiriki michango makanisani.

Viongozi wa kidini wanafaa kutafakari na kujifunza kutoka kwa watangulizi wao wa miaka ya 80 na mapema 90 waliokuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa Wakenya.

Marehemu Nding’i Mwana Nzeki, Maaskofu Manases Kuria, Timothy Njoya, Alexander Muge, David Gitari, Mutava Musyimi na Henry Okullu, waliheshimika kutokana na msimamo wao dhabiti katika kukemea dhuluma zilizoendeshwa na utawala wa Kanu dhidi ya upinzani na raia.

Juhudi za mashujaa hao pamoja na upinzani ndizo ziliwezesha taifa kukumbatia utawala wa vyama vingi.

You can share this post!

OMAUYA: Utawala Tanzania uzingatie haki na demokrasia

Wandani wa Ruto wadai kufungiwa nje ya Jubilee Asili