ODONGO: Heko Raila na Uhuru kwa juhudi zenu kulikomboa Ziwa Victoria
NA CECIL ODONGO
HATUA ya viongozi wakuu nchini kulivalia njuga tatizo la miaka nenda miaka rudi la magugumaji katika Ziwa Victoria ni la kusifiwa sana.
Ikizingatiwa kwamba zaidi ya nusu ya wenyeji wa kaunti nne za Luo Nyanza wanashiriki shughuli za uvuvi ziwani humo, juhudi za Kinara wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta za kupambana na magugumaji zimekuja kwa wakati na kuwapa wavuvi matumaini mapya.
Kama mzaliwa wa eneo la Nyanza, nimeshuhudia jinsi magugumaji yamechangia kuongezeka kwa viwango vya umaskini, wavuvi kupoteza maisha yao na hata wengine kukwama ziwani wakiwavua samaki.
Mwanzo, mmea huu huzua changamoto chungu nzima wakati wa uvuvi kwa kuwa hutatiza usafiri wa boti na pia huzuia wanyama wanaoishi majini kufaidi miale ya jua. Magugumaji haswa huwapa wavuvi taabu wanapotia nyavu zao majini ili kuwanasa samaki.
Athari za magugumaji yameonekana kuchangia kudorora kwa shughuli za kitaalii katika baadhi ya fuo za Ziwa Victoria kama Dunga Hill Camp, Remba na Hippo Point kwa kulemaza usafiri wa watalii ziwani.
Kwa wavuvi, samaki kama ngege na mbuta wamekuwa vigumu kuvuliwa, hali ambayo imepelekea wafanyabiashara na wenye hoteli maarufu kama Kiboko Bay, Eco Lodge, Dunga Hill Camp, Tilapia Resort na Sunset kulalamikia kupungua kwa kitoweo cha samaki kinachopendwa sana jijini Kisumu.
Kukithiri kwa kero la magugumaji ziwani kumekuwa suala ambalo viongozi wa kisiasa kutoka Nyanza wamekuwa wakiahidi kukabiliana nalo wakisaka kura lakini ahadi hizo huishia kuwa maneno matupu mara tu wanapochaguliwa.
Magavana wa Kaunti za Homabay, Migori, Kisumu na Siaya hawakuwahi kuonyesha nia yao ya pamoja ya kutafuta ufumbuzi wa kumaliza mimea hii kabla ya Bw Odinga na Rais Kenyatta kuingilia kati kupambana nayo.
Naamini kwamba magavana hao wangekuwa wamemakinikia kero hili basi wangetenga sehemu za fedha wanazopokea kutoka kwa Hazina ya Kitaifa na kuwatafuta wafadhili ili kuwaokoa wavuvi ambao wamehangaishwa mno na mimea hii.
Wabunge na maseneta wa Nyanza badala ya kushiriki siasa za kumvumisha Bw Odinga na kumkashifu Naibu Rais William Ruto nao wanafaa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi zinazoendelea kwa kuelekeza sehemu ya fedha za CDF katika mradi huu muhimu.
Kulingana na baadhi ya wavuvi niliosema nao mradi huu iwapo utafaulu ndio utakuwa sifa na kumbukumbu zitakazosalia akilini mwao daima dawamu kuwahi kutimizwa na Bw Odinga hata akiamua kustaafu siasa.