Makala

ODONGO: Juhudi za kupatanisha UhuRuto ni kazi bure tu

October 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

KUMEKUWA na madai kwenye vyombo vya habari kuwa juhudi zinaendelea za kuwapatanisha Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2022.

Inadaiwa juhudi hizo zinaendelezwa na baadhi ya viongozi wa kidini ambao wanaona tofauti kali kati ya viongozi hao inaweka nchi hii kwenye hatari ya mgawanyiko mkubwa na mapigano jinsi ilivyokuwa 2007.

Hata hivyo, kulingana na matukio ya kisiasa nchini, ni dhahiri kwamba huenda juhudi hizo zisizae matunda kwa kuwa wawili hao hawajajitokeza hadharani na kutangaza kiini cha kukosana kwao.

Ingawa, wengi wamekuwa wakikisia kuwa ni hatua ya Rais kuanzisha ushirikiano na Kinara wa ODM Raila Odinga, huenda kuna mengine mengi ambayo hayajawekwa hadharani.

Mnamo 2013, ugani Afraha wawili hao walidhihirisha uzalendo mkubwa walipoviunganisha vyama vyao vya TNA na URP licha ya uhasama mkubwa uliokwepo kati ya jamii zao kwenye uchaguzi wa 2007.

Tena kuelekea kura ya 2017, Rais na Naibu wake waliongoza viongozi wengine kuviunganisha vyama vingine 14 na kuibuka na muungano wa Jubilee. Je, kukosana kwao kunamaanisha kwamba umoja huu ulikuwa tu wa kuwahadaa Wakenya ili wachaguliwe uongozini?

Vilevile baadhi wanaweza kufasiri matukio hayo kama hatua ya Rais kumchenga Dkt Ruto kisiasa hasa baada ya kusema hadharani kwamba atamuunga mkono akimaliza muhula wake wa pili.

Licha ya matukio hayo, itakuwa kibarua kigumu kwa viongozi wa kidini kuwaleta pamoja Rais na Naibu. Pengine juhudi hizi zingeanza mapema basi zingeafikiwa kwa kiasi fulani.

Kwanza, tayari Rais Kenyatta amechukua udhibiti wa Jubilee na kuwatema wandani wote wa Dkt Ruto kwenye nafasi za uongozi katika Bunge la Kitaifa na lile la Seneti. Pia wandani wa Rais kama David Murathe na Raphael Tuju bado wanaendelea kudhibiti Jubilee hali inayodidimiza matumaini zaidi ya upatanishi huo ikizingatiwa wamekuwa wakimshambulia sana Dkt Ruto.

Pili, Rais Kenyatta mara nyingi amewarai wanasiasa wasitishe kampeni za 2022, lakini ambaye anaonekana kutotii amri hiyo kabisa ni Dkt Ruto.

Naibu Rais amekuwa akihudhuria ibada kwenye makanisa ya miji mbalimbali kisha kuandaa mikutano ya hadhara katika miji ya karibu na maeneo anakozuru. Haitakuwa rahisi kwake kusitisha mikutano hiyo kwa kuwa anaamini ni njia ya kujiandaa mapema kuteka nyoyo za raia kabla ya 2022.

Aidha juhudi za upatanishi zilizoongozwa na wanasiasa na viongozi wa kidini mara nyingi zimekosa kuzaa matunda miaja

Mnamo 1994, askofu wa ACK marehemu Manases Kuria alijaribu kuwapatanisha Raila Odinga na marehemu Kijana Wamalwa kuhusu mzozo wa uongozi ndani ya Ford Kenya. Hata hivyo, hakufaulu na mwishowe viongozi hao wakaenda njia tofauti.

Kwenye uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mnamo 1992, mwanaharakati wa kisiasa Wangari Mathai pamoja na viongozi wa kidini, walijaribu kuunganisha upinzani chini ya chama cha Ford lakini hawakufaulu. Mwishowe Oginga Odinga, Kenneth Matiba na Mwai Kibaki walishikilia misimamo yao mikali na Rais Daniel Moi akatetea wadhifa wake kwa urahisi.

Kilichoko wazi ni kwamba mara nyingi viongozi wa kisiasa huungana kutimiza malengo yao ya kisiasa na viongozi wa kidini huwa hawatekelezi jukumu muhimu kuwaunganisha ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Hii ndiyo maana licha ya heshima na hadhi yao, si rahisi kwa viongozi wa dini kuwaunganisha Rais na Naibu wake iwapo mmoja kati ya hao anaona hahitaji mwenzake kisiasa.

Juhudi za kuunganisha Rais na Naibu wake pia huenda zikahatarisha udhabiti wa handisheki kati ya Rais Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye pia anaelekeza macho yake na kupima jinsi upepo wa kisiasa wa 2022 unavyovuma.