Makala

ODONGO: Matamshi ya Raila Jr si uasi dhidi ya baba yake

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CECIL ODONGO

HATUA ya mwanawe Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kukemea baadhi ya viongozi wa chama haifai kufasiriwa kama maasi ya kisiasa dhidi ya babake na chama hicho.

Kupitia mtandao Twitter wiki jana, Bw Raila Jnr aliwakashifu baadhi ya viongozi wa ODM kwa kujikita zaidi katika mashambulizi dhidi ya viongozi wa Tangatanga badala ya kuzingatia msingi wa chama kuimarisha utoaji wa huduma kwa raia.

Kama mwanachama wa ODM, Bw Raila Jnr ana kila haki ya kukikosoa iwapo anaona kinaelekea pabaya kwa kutozingatia masuala ya kimsingi ya uongozi.

Demokrasia ambayo Bw Odinga alipigania miaka ya 80 na mapema 90 kabla mfumo wa vyama vingi ukumbatiwe, inampa kila mtu haki ya kutoa maoni yake kuhusu masuala mbalimbali ya nchi.

Kwa hivyo, Bw Raila Jnr hafai kufungwa na minyororo ya ukuu wa babake chamani kiasi kwamba, hawezi kutoa maoni yake anapoona chama kinaelekea visivyo.

Kwa upande mwingine, ni vyema mwanawe Bw Odinga atumie asasi zilizoko chamani kuwasilisha malalamishi yake kabla ya kufoka hadharani.

Hata hivyo, kwa sasa haifahamiki iwapo aliziwasilisha na zikakosa kutiliwa manani au hakuziwasilisha kabisa.

Shutuma za Bw Raila Jnr hata hivyo, zinawaweka pabaya, baadhi ya viongozi wa chama ambao wana mazoea ya kuwataja wenye maoni kinzani kama fuko miaka ya nyuma.

Je, mwanawe Bw Odinga pia ni fuko ndani ya chama au ni mwandani wa Naibu Rais jinsi walivyokuwa wabunge wa ODM kutoka Pwani waliohamia kambi ya Naibu Rais Dkt William Ruto?

Ingawa hivyo, hata kabla ya shutuma za wiki jana, Bw Raila Jnr amedhihirisha si limbukeni katika siasa na masuala tatanishi.

Mnamo 2018, Bw Raila Jnr aliirai serikali iondoe marufuku dhidi ya bangi kama dawa ya kulevya kwa kuwa utafiti wa kisayansi umedhihirisha kwamba, dawa hiyo ni tiba kwa baadhi ya maradhi.

Mapema mwaka huo, pia aliongoza maelfu ya wafuasi wa ODM kumlaki babake kutoka Amerika katika uwanja wa JKIA, tukio ambalo lilihusisha ghasia na makabiliano makali kati yao na maafisa wa usalama.

Pia, Bw Raila Jnr alikuwa kati ya waliomfanyia babake kampeni kali kabla ya uchaguzi wa 2017.

Haya matukio yote yanaonyesha Bw Raila Jnr si limbukeni kisiasa.

Yamkini ameanza kuweka mikakati ya kupigania udhibiti wa chama cha babake ambaye uzee unazidi kumwandama.

Ikumbukwe kwamba, kabla na baada ya uchaguzi wa 1992, Bw Odinga alikuwa mbunge na mkurugenzi wa masuala ya uchaguzi ndani ya Ford Kenya, chama kilichokuwa kikiongozwa na marehemu babake Jaramogi Oginga Odinga.

Baada ya kifo cha babake 1994, Bw Odinga alipigania udhibiti wa chama hicho na marehemu Wamalwa Kijana licha ya kutorokwa na wandani wa Bw Jaramogi kutoka Nyanza kama James Orengo na Profesa Anyang’ Nyong’o ambao walikuwa mrengo wa mbunge huyo wa Saboti.

Huenda, Bw Raila Jnr pia analenga kuiga alichofanya babake akilenga kuwania cheo cha kisiasa 2022 na pia kuwaengua baadhi ya wandani wa babake ambao wamemzingira na wanadhani wao ndio wamiliki wa ODM.

Badala ya baadhi ya wanasiasa au watu kusawiri kauli ya Bw Raila Jnr kama ishara ya maasi, kuna familia ambazo zimegawanyika kisiasa peupe siku za nyuma hata kuliko familia ya Bw Odinga.

Kwenye uchaguzi wa 2017, mbunge wa sasa wa Bomet Mashariki, Beatrice Kones, mkewe Waziri wa zamani marehemu Kipkalya Kones wa Jubilee aliwania dhidi ya mwanawe Kevin Kones aliyegombea kupitia chama cha mashinani.

Katika uchaguzi wa eneobunge la Jomvu mnamo 2013, mbunge wa sasa Twalib Badi aliwania dhidi ya Seif Kajembe ambaye ni nduguye mkewe.

Katika taifa jirani la Uganda, Godfrey Kimera anayepanga kutetea uchaguzi wa manispaa ya mji wa Kasaali 2021, aliapa na kumkataa mwanawe wa damu Reginah Nakiweewa hadharani baada ya kugundua alikuwa akilenga kumpinga kwenye kura hiyo.

Kwa hivyo, hata iwapo suala la Bw Raila Jnr litatokea hatimaye kuwa la maasi dhidi ya babake, basi halitakuwa suala geni.

Kilichoko muhimu ni kwamba, masuala anayoyaibua kwa sasa kuhusu seneti na ODM yana mashiko.