ODONGO: ODM yatumia vita dhidi ya ufisadi kujikweza kisiasa
Na CECIL ODONGO
NI bayana kwamba, Chama cha ODM kinahadaa Wakenya kwamba kinamakinika kupambana na ufisadi ilhali kinatumia uovu huo kuendeleza ajenda za kisiasa.
Msimamo wa ODM kuhusu vita dhidi ya ufisadi sasa haueleweki kutokana uvuguvugu ambacho chama kimekuwa kidhihirisha katika hali tofauti.
Katika tukio la kushangaza, chama hicho kiliandaa mkutano wa dharura na kuwaamrisha madiwani wawasilishe hoja ya kutokuwa na imani na Gavana wa Migori, Zachary Okoth Obado. Bw Obado alishtakiwa pamoja na watu wengine kwa ubadhirifu wa Sh73 milioni za kaunti katika kipindi cha matumizi ya fedha cha 2013/14.
Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi na Katibu Mkuu Edwin Sifuna waliwaalika madiwani jijini Nairobi na kuwashawishi wamwondoe Bw Obado uongozini ingawa kesi dhidi yake ilikuwa imeanza wala hakupatikana na hatia.
Kati ya masuala waliyoyataja viongozi hao wa ODM ni kwamba, korti ilimzuia Gavana huyo kutia guu afisini na pia uhusiano mbaya kati yake na Naibu Gavana Nelson Mahanga haungehakikisha wananchi wanapokea huduma nzuri.
Ingawa wafisadi wanafaa kukabiliwa vikali nbila huruma, si vyema Bw Obado apokezwe adhabu na ODM ilhali kesi yake haijakamilika wala hajapatikana na hatia.
Kwanza, Bw Obado anafaa ajiuzulu kivyake iwapo anaona hataweza kuwajibikia raia vyema kutokana na kesi inayomkabili mahakamani.
Pili, ni dhahiri ODM haijawahi kuridhia uongozi wa Bw Obado tangu achaguliwe Gavana 2013.
Kwenye uchaguzi huo, Bw Obado alimwabaga mgombeaji wa ODM Profesa Akong’o Oyugi na kutwaa kiti cha ugavana kupitia PDP baada ya kudai alichezewa shere kwenye kura za mchujo.
Si jambo la siri kwamba, eneo la Luo Nyanza ambako ODM ni maarufu, baadhi ya viongozi wanaopendwa na wananchi hutupwa nje kwenye mchujo na tiketi kukabidhiwa wanaopendelewa na ‘wakubwa’ chamani.
Aidha uhasama wa ODM na Bw Obado ulitokota zaidi mnamo Septemba 2014, alipoongoza ujumbe wa watu 600 uliowajumuisha vijana, akina mama na wazee kufika katika Ikulu ya Nairobi kumwomba Rais Uhuru Kenyatta msamaha.
Mnamo Aprili 2017 mkutano wa ODM mjini Migori uliohudhiriwa na Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o, Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Hassan Joho wa Mombasa ulitibuka na baadhi ya walinzi wao kujeruhiwa.
Wakati huo, Bw Obado alilaumiwa kwa kutumia makundi ya vijana kuvuruga mkutano huo kutokana na madai viongozi hao walipinga uwaniaji wake wa kiti cha ugavana.
Isitoshe mwaka huo alirejea ODM na kumbwaga Seneta wa sasa Ochillo Ayacko kwenye kinyang’anyiro cha ugavana 2017.
Ni dhahiri kwamba, Bw Obado amekuwa akivuma kisiasa kutokana na nguvu za wananchi wala si kwa mapenzi ya ODM. Hii ndiyo sababu wakuu wa ODM wanatumia masaibu yake kutaka aondoke uongozini ili kuweka kiongozi mtiifu kama wanaotoka kaunti za Kisumu, Siaya na Homa Bay.
ODM inafaa kuwa na msimamo wa wazi kuhusu vita dhidi ya ufisadi badala ya kutumia kampeni hiyo kuadhibu viongozi wanaonekana kuwa waasi na kuwasaza wengine.