ODONGO: Rivatex ichangie katika ufufuzi wa kilimo cha pamba
Na CECIL ODONGO
KUFUFULIWA kwa kiwanda cha kutengeneza nguo cha Rivatex kumewapa matumaini mapya wakulima wa pamba kutoka iliyokuwa mikoa ya Nyanza, Bonde la Ufa na Magharibi.
Kiwanda hicho kilichofunguliwa upya na Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa iliyopita kilisifika miaka ya themanini na tisini kwa kutengeneza nguo na kubuni nafasi nyingi za ajira kwa Wakenya.
Tunaposifia kufufuliwa kwa Rivatex, ni vyema kuhakikisha kwamba matatizo yaliyoizonga miaka ya nyuma na kusababisha kuporomoka kwake hayarejelewi ili mara hii ifane katika utendakazi wake.
Hata hivyo, ufanisi huo utafikiwa tu iwapo serikali itatekeleza mikakati kadhaa ambayo ikitiliwa manani basi kiwanda hiki kitafanikisha maazimio yake nchini.
Kwanza, serikali inafaa kuhakikisha kwamba maafisa wakuu wa kiwanda hiki ni watu wenye maadili na wasiojawa na tamaa ya kufuja mali ya umma wakiwa uongozini.
Imebainika kwamba viwanda vilivyoporomoka na kushindwa kurejea ulingoni kama Mumias na Webuye vilianguka kutokana na uongozi mbaya na wasimamizi wafisadi, ambao baadaye walijiuzulu na kutumia mali waliyoiba kuyoyomea katika siasa.
Vile vile wanasiasa pia wasiruhusiwe kuingilia usimamizi wa kiwanda cha Rivatex kwa sababu watatumia ushawishi wao kuhakikisha washirika wao wanaajiriwa na wengine wanashikilia nafasi za juu kiwandani, kisha kuwatumia kukifilisi kifedha hasa nyakati za kampeni.
Pili, maslahi ya wakulima ambao watakuwa na mchango mkubwa katika uendeshaji wa Rivatex kwa kushiriki kilimo cha pamba yaangaliwe vizuri na serikali.
Kwa sasa ni ukweli kwamba kilimo cha pamba kimekufa hasa katika maeneo yaliyosifika kwa ukuzaji wa mmea huo kama Nyando, Kisumu, Nyanza Kusini na maeneo mengine ya Bonde la Ufa na Magharibi mwa nchi.
Itailazimu serikali kuwahamasisha wakulima, ambao wengi wao bado wanauguza machungu ya kutolipwa fedha kwa pamba walizowasilisha kwa kampuni za KIKOMI mjini Kisumu na Rivatex, kurejelea kilimo cha pamba.
Uhamasisho huo unafaa kujumuisha hakikisho kwamba wakulima hawa watalipwa malimbikizi wanayodai Kikomi na Rivatex, kisha waafikiane na usimamizi wa kampuni hizo kwamba watakuwa wakilipwa kila mara wanapowasilisha pamba badala ya mtindo wa zamani walipolazimishwa kusubiri kupokea fedha zao baada ya miezi kadhaa.
Tatu, jinsi alivyosema Rais Kenyatta, Rivatex inafaa ianze kuzamia matangazo ya nguo na mavazi mengine inayotengeneza ili Wakenya wayanunue.