Makala

ODONGO: Seneti izingatie haki iketipo kuamua hatima ya Sonko

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

BUNGE la Seneti linafaa kutathmini kwa undani madai yatakayowasilishwa kuunga hatua ya madiwani kumbandua Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko.

Gavana huyu alibanduliwa uongozini wiki jana baada ya madiwani 88 kuunga mkono hoja ya kumtimua huku wawili pekee wakipinga.

Japo, amepinga kutimuliwa kwake kwa kuwasilisha kesi kortini akisema shughuli hiyo haikufuata sheria, ni wazi kwamba uamuzi wa Seneti ndio utaamua hatima ya Sonko.

Kamati itakayobuniwa kuchunguza madai dhidi yake inafaa kujikita katika kuchunguza ufisadi dhidi yake na kiini cha uhusiano uliozorota kati ya mbunge huyo wa zamani wa Makadara na Mkurugenzi wa Shirika la Huduma za Jiji Mohammed Badi.

Pia, Seneti inaweza kuamua Bw Sonko ajitetee mbele ya maseneta wote jinsi ilivyokuwa kwa aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu ingawa jambo muhimu ni ukweli ubainike kuhusu masuala yatakayoibuliwa na yaamuliwe kwa haki.

Si siri kwamba siasa za ‘handisheki’ huenda zikaamua pakubwa hatima yake iwapo Bw Sonko atajitetea mbele ya kamati ya Seneti au maseneta wote.

Hata hivyo, huenda shutuma kali ambazo seneta huyo wa zamani amekuwa akitoa dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta zikamchongea na kusababisha kutimuliwa kwake.

Baada ya kusaini mkataba wa kuachia baadhi ya majukumu yake kwa NMS mnamo Januari mwaka huu, Bw Sonko amekuwa vuguvugu mara akiridhiana na Bw Badi kisha wakati mwingine akimshutumu. Aidha, hata amewahi kudai kwamba alisaini stakabadhi za kuhamishia NMS majukumu katika Ikulu baada ya kupewa pombe.

NMS

Ukweli ni kwamba japo hatua ya kukabidhi NMS baadhi ya majukumu ilikuwa kwa manufaa ya wakazi wa Nairobi, sawa na kiongozi yeyote, alihisi kwamba amedhulumiwa licha ya raia wengi kuwa na imani naye ndiposa wakampigia kura mnamo 2013.

Vilevile, alihisi kudhulumiwa zaidi baada ya madiwani kutenga Sh37 bilioni kwenye bajeti ya kaunti kwa NMS na kumwacha na Sh8 bilioni pekee ambazo zisingetosha kufanya makuu.

Maseneta wa upande wa ‘handisheki’ wanaounga mkono mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga wana idadi tosha ya kuidhinisha kubanduliwa kwa Bw Sonko na watafasiri shutuma zake dhidi ya NMS na Rais kama mwanasiasa anayepinga serikali.

Pia, anachongewa zaidi na matamshi yake ya kwamba kwa sasa Wakenya wanahitaji kupokezwa huduma bora badala ya wanasiasa kurindima ngoma ya BBI. Matamshi hayo yamekuwa yakifasiriwa kuwa yeye yupo mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye ameonyesha uvuguvugu kuhusu BBI.

Ikumbukwe kwamba siasa za handisheki zilimwokoa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru baada ya kutimuliwa na madiwani wa kaunti hiyo kwa madai ya utawala wake kugubikwa na ufisadi.

Kwa Bw Sonko, itakuwa vigumu kunusurika hasa akilaumiwa kwa kutomteua Naibu Gavana tangu kubanduka kwa Polycarp Igathe mnamo Januari 2018.

Pia Gavana huyo amelaumiwa kutokuwa na uhusiano mzuri watu anaowateua kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali, akiwafuta kiholela wanapotofautiana.

Ingawa hivyo, seneti inafaa kusimamia haki na kuchunguza madai dhidi yake kwa undani.