• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
ODONGO: Vyama vya wafanyakazi vimeshindwa kutetea wanachama

ODONGO: Vyama vya wafanyakazi vimeshindwa kutetea wanachama

NA CECIL ODONGO

DALILI zinaonyesha kwamba miungano mbalimbali ya kuwatetea wafanyakazi nchini imepoteza makali yake na sasa haiwezi kupigania maslahi ya wanachama wao kwa ujasiri kama ilivyokuwa miaka ya awali.

Hii ni baada ya viongozi wake kuingia kwenye siasa, baadhi wakimezwa na serikali na kukosa ukakamvu wa kuwatetea wafanyakazi.

Miongoni mwa maafisa wanaosimamia vyama vyao na wakati huo huo ni viongozi wa kisiasa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Nchini(KNUT) Wilson Sossion, Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba ambaye ni Mwenyekiti wa Mungano wa Walimu Wa Shule za Upili (KUPPET), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Bungoma Catherine Wambilyianga na Mbunge wa Bomet ya Kati Ronald Tonui ambao wanashikilia nyadhifa Kuppet.

Pia kuna Tom Odege wa Chama cha Wafanyikazi wa Umma.

Uwepo wa viongozi hao bungeni haujasaidia kusukuma ajenda za wafanyakazi jinsi ilivyotarajiwa.

Kati ya hawa wote ni Bw Sossion pekee ambaye ameonekana kuendeleza uanaharakati kwa kupinga utekelezaji wa mtaala mpya na sera kandamizi za Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC).

Hati hivyo, Bw Sossion amejipata pabaya kutokana na juhudi hizo baada ya tume hiyo kuliondoa jina lake kwenye sajili ya walimu na pia kukosa kuwasilisha michango ya wanachama kwa muda wa miezi miwili kwa Knut, hali ambayo imelemeza shughuli za chama hicho.

Walimu wanachama wa Knut nao wamekosa kupokea nyongeza waliyoahidiwa kwenye makubaliano kutokana na uadui kati ya chama chao na serikali.

Kwa sasa Knut ipo kwenye mkondo wa kusambaratika serikali ikitumia mbinu ya kugawanya miongoni mwa maafisa wake, ambao baadhi sasa wameanza kupiga ngoma ya kumwondoa katibu wao.

Isitoshe, Muungano Wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) chini ya Katibu Mkuu Francis Atwoli nao unaonekana kupoteza dira na kusahau jukumu lake kuu la kupigania maslahi ya wanachama wake kote nchini.

Bw Atwoli mara nyingi amekuwa kwenye vyombo vya habari sio kwa sababu ya kuwatetea wafanyakazi mbali kupiga siasa za 2022, akipinga vikali azma ya Naibu Rais William Ruto ya kuingia ikulu.

Hakuna chochote cha maana COTU kimeafikia tangu serikali ya Jubilee iingie mamlakani, mara nyingi wafanyakazi wakikosa hata nyongeza ya mishahara ya kila mwaka siku ya Leba Dei inapoandaliwa.

Kwa kuwa maafisa wanasiasa wameshindwa kupigania vilivyo maslahi ya wanachama wao, ni vyema vyama hivi vitathmni kutowaruhusu wanasiasa kuvisimamia siku zijazo, na pia viwe na maafisa wenye ujasiri wa kuwateta kwa kila hali na mali.

You can share this post!

WANDERI: Jubilee ikome kutumia kifua dhidi ya Wakenya

MBURU: Raia wahamasishwe kuhusu athari za uchafuzi wa mito

adminleo