Ole wako unayebusu jamaa mwenye ndevu, bakteria zinakusubiri
DAKTARI na mtaalamu wa afya Dkt Myro Figura ametahadharisha dhidi ya kupiga busu wanaume wenye ndevu, akisema hatua hiyo inaweza kukusababishia maambukizi na mwasho kwa ngozi.
Kutokana na hilo amewataka wanaume au wanawake wanaobusu wanaume wenye ndevu wajihadhari kwa sababu hiyo ni njia moja ya kujiletea maradhi.
“Kupiga busu mwanamume mwenye ndevu kunaweza kukusababishia maradhi. Iwapo ndevu zenyewe si safi huwa ni hifadhi ya bakteria, na wakati wa kupiga busu vijidudu hivyo hatari vikitagusana na ngozi basi huleta upele wa malengelenge (impetigo kwa Kimombo),” asema Dkt Figura.
Impetigo ni ugonjwa ambao unasambaa kwa urahisi.
Huanza kwa ngozi kuwa na uvimbe kisha kutoa uchafu mwekundu.
Mara nyingi uchafu huo ambao ni majimaji si rahisi kutambuliwa kwa watu wenye ngozi nyeusi au rangi kahawia.
“Uvimbe ukipasuka huacha vidonda vidogo na husambaa sehemu mbalimbali za mwili. Kibaya zaidi ni kuwa aliyeathirika hujikuna sana na kuhisi uchungu kutokana na mwasho,” aongeza mtaalamu huyo katika utafiti uliochapishwa kwenye jarida la habari la Daily Mail nchini Uingereza.
Tiba ya maambukizi haya ya bakteria ni kupaka mafuta yenye kemikali ya hydrogen peroxide ama kumeza tembe za kukabiliana na bakteria mwilini.
Ushauri wa daktari utafaa kumaliza bakteria hizi, ila cha mno ni kwa wanaume kuhakikisha kuwa ndevu zao ni safi na pia nywele zilizo sehemu zingine za uso zinaoshwa.
Kufutia utafiti huo wa Dkt Figura na video aliyochapisha mitandaoni, wanawake wengi walimuunga mkono na hata kudakia suala hilo kama kisababu cha wao kuepuka wanaume wenye kidevu.
Wengine walishangaa kwamba wanaume huwaoshi ndevu zao mara kwa mara, huku wale ambao midume yao ina kidevu wakiapa kuwafuatilia ili kuhakikisha wanaosha nywele hizo kisawasawa.