Makala

OMAUYA: Ibilisi tuliyemuumba kwa kubagua vijijini sasa atutafuna

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MAUYA OMAUYA

Ulisikia wapi? Ulisikia wapi eti jogoo wa shamba hawiki mjini?

Ndivyo sivyo, sivyo ndivyo, mambo hubadilika.

Na wanavyosema kina yakhe, vindu vichenjanga!

Ikiwa kuna jambo limeendelea kubainika wazi kuhusu ujenzi wa taifa, ni msemo huu wa huko vitongojini, “mambo ni mawili, tusipokula utajiri wako sote, itabidi tule umaskini wangu sote.”

Kitoweo cha taifa la Kenya kipo mijini. Tangu uhuru, mamilioni wamekisaka kwa kurundikana mijini – Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru. Sehemu nyingi mashinani zimesalia mahame na vichaka visivyotamanika. Hili ni kosa la kihistoria. Tunaendelea kushuhudia upofu huu katika mvutano kuhusu ugavi wa mapato ya nchi kwa majimbo kwenye Bunge la Seneti, ujinga ulioje? Labda funzo lipo kwenye adhabu tunayoendelea kupitia mikononi mwa janga la corona.

Wimbi hili limetetemesha sana miji mikuu iliyotazamiwa kuwa kilele cha maendeleo ya usimamizi wa serikali; ufanisi wa teknolojia; kitovu cha ajira; kianzo cha utamaduni wa kisasa; makazi safi, kazi, afya, chakula, maji, mavazi, burudani, elimu ya juu na maono ya siku zijazo.

Yaani kila tunachotamani maishani, kumbe kimefichwa mijini! Makosa sana! Maelfu ya raia walioshindwa kustahimili moto wa Corona jijini Nairobi na miji mingine waligeuza macho yao kutafuta wokovu mashambani! Watoto, wanafunzi na wasio na kazi mijini wamerushwa mashinani ili kupunguza gharama ya maisha inayozidi kufinya mamilioni ya Wakenya. Waliobakia mijini wameendelea kutegemea vijiji hata kwa lishe. Hatimaye tunakumbana na ibilisi tuliyemuumba kihistoria kwa kubagua maeneno ya mashambani tunapojenga taifa.

Kumbe mipaka ya nchi ikifungwa tunakumbuka ladha ya boilo kutoka Suguta Marmar, Samburu kwa sababu hatupati viungo vya Pizza ya Margarita kutoka Bologna, Italia?

Kumbe jiji linapokuwa halikaliki, tunatorokea mashinani, tunazamia kuteka maji mitoni, kuisafirisha vichwani au kwa punda, kupitia vijia au barabara mbovu hadi mabanda yetu ya nyasi vijijini? Jogoo wa jiji amefika shambani.

Na kumbe usiku wetu vijijini ni mrefu, uliojaa mateso ya giza, minong’ono ya mbu na bundi au kimya cha kutisha kwa sababu hakuna dalili za nyaya za stima? Vizuri tu!

Mambo haya sio mageni; macho yetu ndio yaliyopofuka, masikio yetu ndio yaliyoziba na akili zetu kudinda kujifunza kutokana na historia ya mataifa. Lazima tuelekeze ustawi wa kiuchumi mashinani pia. Tumekwama kwenye tope la maangamizi ikiwa tunaendeleza kosa la kuwekeza nguvu, maarifa na ndoto za vizazi vyetu katika kuinua miji ilhali mashinani hali ni shaghala baghala! Tukizidi kupanua pengo kati ya jogoo wa jiji na jogoo wa shamba, tutajuta kama taifa.

[email protected]