• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
OMAUYA: Masaibu ya Sonko ni mwiba wa kujidunga, hauambiwi pole!

OMAUYA: Masaibu ya Sonko ni mwiba wa kujidunga, hauambiwi pole!

Na MAUYA OMAUYA

MAZOEA yana tabu!

Katika kuzoea kuna raha ya kusahau. Katika kusahau kuna hatari ya kutozingatia hekima. Katika kutozingatia hekima, raha hugeuka karaha. Hii ndiyo historia ya Gavana Mike Sonko wa Nairobi baada ya kura ya kumng’oa mamlakani kufaulu.

Gavana Sonko ataanguka kwa mshindo mkuu kwa sababu pia alipanda na kupaa kwa mshindo. Ikumbukwe kwamba akiwa juu mawinguni alitetemesha uwanja wa siasa Nairobi kwa kila aina ya madaha, mikogo, mbwembwe na bling’ bling’ zisizofaa.

Basi, kishindo cha kuporomoka kwa himaya yake kitasalia funzo kuu kwa kina yakhe kwenye siasa. Funzo hili ni kama la Ikarus mwanawe Daedalus!

Kwa miaka na mikaka, hadithi ya kijana aitwaye Ikarus na babake Daedalus kutoka Ugiriki ya zamani imesimuliwa. Hata hivyo, ladha ya simulizi haijapungua na mafunzo ya kisa yangali na hadhi hata baada ya karne kadhaa.

Daedalus, aliyekuwa fundi na mbunifu hodari na mwanawe Ikarus walikuwa wafungwa katika kisiwa cha Krete. Baba akang’amua na kubuni mpango mwafaka kutoroka madhila yao katika gereza la upweke. Kwa kutumia nta na manyoya, mzee Daedalus aliunda mabawa ili waondoke kisiwani kwa kupaa kama ndege angani. Ilikuwa zamani sana, kabla watu hawajagundua usafiri wa mashua au meli.

Kabla ya kung’oa nanga, Daedalus alimuomba Ikarus aepuke mambo mawili. Kwanza, alimtaka awe mwangalifu ajitenge na ‘mazoea’ yaani kuridhika kuwa mambo yote yako shwari na yatazidi kuwa shwari. Katika hali hii ya mazoea, mtu hawezi kujirudi au kujikosoa.

Pili, mzee alimuonya mwanawe dhidi ya mtego wa wingu hatari la kiburi, tabia inayojulikana kama hubris kwa lugha ya Kigiriki. Kiburi humpofusha mtu asione, asisikie wala kufuata hekima. Mtu mwenye hubris anaamini uwezo wake, hukataa mwongozo au mawaidha na hujiona mkuu kuliko kila kiumbe. Hatimaye hubris humfanya mtu kukaidi na kudharau miungu. Hilo lilikuwa kosa kubwa katika jamii ya enzi hizo, hata leo.

Ili kudumisha usawa wa mbawa, Daedalus alimsihi Ikarus asiruke juu sana karibu na jua au chini sana palipo na bahari. Joto la jua na maji ya bahari, viwili hivi vingedhuru mbawa zake. Alitakiwa aruke kwa kufuata mkondo na mwelekeo wa babake. Safari ikaanza.

Ukaidi

Akiwa angani, Ikarus aliona raha ya kupaa kama ndege, ilikuwa starehe ya ajabu. Alijipinda kushoto, kulia na kujibingirisha kwenye mawimbi kwa madoido kama afanyavyo mwewe. Kiburi kilimteka akajitanua kifua, akapaa juu, juu zaidi karibu na jua kinyume na maagizo ya babaye.

Joto kali la jua likayeyusha nta zilizoshikilia mbawa. Alipigapiga mikono hewani akitapatapa lakini wapi, alikosa pa kushikilia akaanguka na kuangamia majini kwa kishindo puuh! Hadi leo bahari hiyo inaitwa Ikarus. Pia kisiwa kilichoko karibu kimepewa jina lake kama kumbukumbu ya ujinga wa Ikarus.

Yaliyompata Ikarus, yamempata Sonko. Akiwa kileleni, Gavana huyu alipuuza hata mwito wa kuteua naibu wake, akakiuka mkataba na wapigakura, akasimanga viongozi, akapuuza Rais na zaidi ya yote akaongoza taasisi za umma kama kioski chake mwenyewe. Hatimaye joto lilipozidi, dakika ya mwisho alidhani atatia usimamizi wa kaunti kikapuni aishie Pwani kwa raha zake. Ndoto yake imevunjika. Mazoea yana tabu kweli. Msiba wa kujitakia hauna kilio.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Seneti izingatie haki iketipo kuamua hatima ya Sonko

Mirengo ya BBI yaanza kumtia Ruto kiwewe