• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
OMAUYA: Serikali isaidie kurejesha ladha ya kilimo cha majani chai

OMAUYA: Serikali isaidie kurejesha ladha ya kilimo cha majani chai

Na MAUYA OMAUYA

MASHIRIKA yanayodhibiti na kuendesha kilimo cha chai nchini Kenya yanahitaji mageuzi ya haraka.

Kilimo hiki hakiwezi kustawi iwapo tutazidi kusafiri njia ya maangamizi hata baada ya kupata mafunzo kutokana na historia ya kahawa na miwa.

Chai ni kitega uchumi cha daraja la juu zaidi humu nchini. Chai inaongoza katika vyote ambavyo vinazolea Kenya mapato kutoka nje mwa nchi.

Mwaka uliopita Kenya ilivuna Sh20 bilioni hela za kigeni kutokana na zao hili. Asilimia 23 ya mapato ya taifa hili hutokana na chai. Wengi wanaochangia zao hili ni wakulima wadogo wadogo mashinani. Kilimo hiki kinategemewa na zaidi ya watu milioni tano nchini.

Isitoshe, taifa hili linaongoza kote duniani katika uzalishaji wa majani chai nyuma ya mabingwa China, India na Sri Lanka.

Hata hivyo, licha ya utajiri mkubwa unaopatikana kutoka kwa zao hili adhimu, wakulima kote nchini wamezidi kutamaushwa huku sekta hiyo ikidorora na wengi wao kuachwa hohehahe, wasio na mbele wala nyuma.

Inavunja moyo zaidi kubaini kwamba tatizo linalolemaza sekta hii ni usimamizi mbaya na ufyonzaji wa wachache wanaovuna wasichokipanda.

Shirika la KTDA linadhibiti asilimia 60 ya mauzo ya chai na kuwakilisha idadi kubwa ya wakulima wadogo wadogo. Utepetevu wa usimamizi na magenge ya watapeli katika utendakazi wa shirika hili umeletea wakulima hasara isiyo na kifani. Sekta iliyokuwa fahari ya Kenya imegeuzwa kuwa sinia ya mabwanyenye walafi wanaodhulumu wakulima maskini.

Viwanda vya chai vilivyokuwa kimbilio mashinani vimetekwa na wasimamizi waliojaa ubinafsi. Kilimo cha chai hakina ladha tena kwa raia wa kawaida.

Majuzi tumeshuhudia wakulima waking’oa mimea yao kufuatia hasira ya hasara wanayopata. Inapofikia kwamba mwaka 2020 mkulima analipwa Shilingi tisa pekee katika bonasi kwa kila kilo moja ya zao lake, basi fahamu utapeli huu umevuka mipaka na chombo hiki kinaelekea kuzama.

Ikumbukwe KTDA huuza kilo ya majani chai kwa angaa Sh400 nje ya nchi. Shilingi tisa kwa mkulima ni dhuluma.

Matatizo yanayokabili zao hilo yalitangazwa wazi na waziri wa kilimo Peter Munya mapema mwaka 2020.

Waziri alipendekeza sheria itakayokabili magenge ya wafyonzaji na kulainisha usimamizi. Ilivyo sasa ununuzi na uuzaji wa zao hili umegubikwa na usiri, ufisadi na malipo yasiyoeleweka kwa mkulima mashinani. KTDA imepinga mageuzi.

Kwa kupinga mageuzi yanayopendekezwa na Waziri Munya kupitia amri ya mahakama, KTDA imeibuka kuwa kizingiti dhidi ya wakulima. Linalofaa sasa ni mapinduzi kwenye usimamizi huo.

Serikali isisite kufanya hivyo ili kutetea fahari ya nchi na raia wake.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ifikirie upya ufunguzi wa shule

ODONGO: Mvutano wa wanasiasa juu ya IEBC ni njama kuidhibiti