Makala

O'MAUYA: Usafi: Tupate mafunzo kutoka taifa jirani la Rwanda

October 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MAUYA O’MAUYA

TATIZO la Kenya sio uhaba wa sheria za kulainisha utenda kazi na maisha ya raia, sheria ziko nyingi, tena nzuri.

Tatizo la Kenya sio ukosefu wa viongozi wenye maono makuu ya kustaarabisha nchi, viongozi wenye hekima wapo, japo hawatambuliki. Tatizo la Kenya sio uchache wa sala au dua kwa Mola, Wakenya wanasali mno usiku na mchana katika kila kituo cha uhai wao. Tatizo la Kenya ni utamaduni wa uozo uliokita mizizi kwenye mawazo ya watu na taasisi za umma.

Haiwi Jambo geni basi wakati kinara wa Nairobi Metropolitan, Jenerali Mohammed Badi anapotangaza kwamba wakazi wa jiji la Nairobi watahitajika kisheria kushiriki katika shughuli za kusafisha jiji.

Wanaojua wanasema Deja Vu yaani hakuna kipya. Juhudi kama hizo zimekuwepo na zikaambulia patupu kwa sababu ya uozo niliotaja awali, kwa sababu juhudi zenyewe zimejengwa katika misingi ya historia ya ufisadi jijini na kuzingirwa na makali ya ubinafsi.

La zaidi ni kwamba raia wamepofuka na utamaduni wa kutojali kufuatia miaka mingi ya ndoto zilizovunjika. Yaani kupambana na mirundiko ya takataka jijini Nairobi ni sawa na kukabili mirundiko ya ufisadi jijini Nairobi na kote nchini Kenya.

Ni vita vigumu kwa sababu vinahitaji pia mapambano dhidi ya utamaduni uliopo, yaani kushinda vita katika mawazo na nyoyo za raia. Kibarua kigumu!

Unapoona watoto wakicheza kwenye vijito vya maji taka au vilima vya kinyesi; unapoona kina mama wakifua nguo kwenye uchafu wa mto Nairobi, unapoona mabomba ya maji yameziba kwa plastiki, unapoona familia zinaishi kwenye majaa na mirundiko ya taka kule Dandora; unafahamu historia ya uchafu uliokolea jijini Nairobi na ugumu ulio kwa Jenerali Badi kutekeleza sheria za kung’arisha mji.

Gavana Mike Sonko alianzisha mpango wa ‘Ng’arisha jiji’ lakini shughuli zilikwama pindi tu Sonko mwenyewe aliponaswa na kesi za ufisadi. Inasikitisha zaidi kuwa shughuli nyingi ziliendeshwa kama kampuni ya Gavana kupitia Sonko Rescue Team.

Hata Rais Kenyatta amewahi kujitosa katika shughuli za kusafisha jiji lakini wapi!

Hata hivyo ikumbukwe kuwa hatua kama hii imefaulu kwingine na yawezekana Badi amepata msukumo na mfano kutoka kule. Tujifunze nini kutoka Rwanda? Jiji la Kigali nchini Rwanda ni la kupigiwa mfano.

Ndilo Jiji safi zaidi Afrika likiwa kwenye ligi ya Windhoek, Namibia na Tunis, Tunisia. Usafi wa Kigali umeibuka kupitia mwito wa ‘umunsi w’Umuganda’ yaani mchango wa jamii.

Tangu mwaka wa 2009, Umuganda ni siku rasmi ambayo raia wa Rwanda hutumikia taifa katika masuala kama usafi wa miji na vijiji. Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni siku ya Umuganda na ni holidei.

Kila mwananchi aliye Na afya nzuri wa kati ya umri wa miaka 18 na miaka 65 LAZIMA ashiriki! Katika kutekeleza sheria nchini Rwanda serikali ya Rais Kagame haitaki mzaha.

Jumamosi ya Umuganda ifikapo, viongozi kupitia nyumba kumi wako macho Na wako mbele. Kuanzia saa mbili hadi saa tano asubuhi nchi huzimwa; hakuna duka kufunguliwa au gari kuendeshwa barabarani. Kila raia anasafisha mtaa wake. Hata Rais anashiriki. Ole wako polisi wakupate unakwepa jukumu! Kazi ngumu na faini ni dola $6.

Ni sheria nzuri lakini imefaulu kwa sababu kwa raia wa Rwanda imekuwa utamaduni, ni kawaida kiasi kwamba wanasubiri siku hiyo kwa hamu. Je, itawezekana Nairobi?