• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
OMAUYA: Wakati wa Museveni kuondoka sasa umefika

OMAUYA: Wakati wa Museveni kuondoka sasa umefika

Na MAUYA OMAUYA

WAPIGANAJI wa NRA wakiongozwa na Yoweri Kaguta Museveni waliingia na kuteka jiji la Kampala kwa nguvu za risasi na vishindo vya vifaru mapema Januari, 1986.

Walivunjavunja ngome na kumpindua Tito Okello aliyekuwa ikuluni.

Museveni alipoapishwa kuwa Rais tarehe 29 Januari 1986, mbunge na msanii Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) alikuwa kijitoto kidogo cha umri wa miaka minne kwenye mtaa wa mabanda wa Kamwookya, mjini Kampala.

Ni Karne ya 21 sasa, mwaka ni wa 2020, miaka 34 baadaye na Bobi Wine anamkabili Museveni yule yule kwenye kinyang’anyiro cha damu na machozi cha urais.

Inakeketa maini zaidi ukizingatia mbinu za kikatili anazotumia Museveni kushikilia mamlaka na kuadhibu wapinzani wake.

Miaka ya mwanzo, Museveni alipokelewa kama mwanamageuzi aliyekuwa na maono ya ufanisi na umoja wa kitaifa. Alipambana na kuzima vikosi vya makachinja na waasi wa kikabila hasa Kaskazini mwa nchi. Alifaulu kufagia mabaki ya uozo wa Idi Amin na Milton Obote na kuzima makali ya waasi wa kundi la LRA chini ya Joseph Kony.

Alipotwaa ikulu alitangaza sera ya hoja kumi kuu kwa raia wa Uganda; demokrasia halisi kuanzia mashinani inayowapa wananchi nguvu kuelekeza jamii zao, usalama kutokana na ghasia za vikosi vya watawala, haki na usawa kwa jamii na makabila yote.

Zaidi ya haya, alitangaza vita dhidi ya ufisadi, unyanyasaji kutoka nje na akaapa kuongoza mataifa mengine ya Afrika kung’oa mizizi ya madikteta.

Kufikia mwaka wa 1996, Museveni alisifika kama kielelezo cha utawala mpya Afrika. Kwa kinywa chake mwenyewe, alikashifu viongozi walionata mamlakani na kudinda kustaafu.

Alijivika joho la ukombozi na miaka kadhaa baadaye tamaa ya ukuu ikateka mawazo yake na anaelekea kuambulia kwenye ligi ya madude kama Mugabe, Mobutu, Mubarak, Bongo na Gaddafi. Madikteta hawa wa Afrika walikuwa na imani potovu kwamba wao ni wakombozi na taifa haliwezi kuendelea wasipokuwepo.

Kiongozi yafaa aelewe nafasi yake ni kama jukwaa tu katika tamthilia ya maisha na taifa lake. Yapaswa achukue fursa yake jukwaani, atimize majukumu na wakati ukifika aondoke jukwaani pasipo na ati ati.

Nelson Mandela ni shujaa mkuu wa ukombozi ambaye alifahamu wakati wa kujiondoa jukwaani. Hatua hiyo pekee imehakikisha jina lake litazidi kutukuka hata kwa vizazi vijavyo.

Hakuna sera mpya au mwamko wa kipekee ambao Rais Museveni atazindua kwa sasa. Mawazo yake yamechakaa na kila uchao hata chembe kidogo cha ruwaza aliyokuwa nayo inazidi kuzorota.

Kwa kuvuruga katiba ya Uganda, alihakikisha vyama vya kisiasa havina mashiko nchini humo na kupitia asasi za jeshi na polisi amehangaisha uhuru wa kukusanyika na kujielezea. Tazama jinsi alivyozima nyota ya Kizza Besigye. Baada ya kupanua mihula, sasa ameondoa hata kizuizi cha umri kwa urais.

Unapozingatia miereka ya kisiasa kati ya Museveni na Bobi Wine, historia itamkejeli Museveni na kumtia kapu moja na Mfalme Louis XIV wa Ufaransa aliyeongoza nchi kwa miaka 72. Kipindi hiki kilikuwa kirefu mno hadi aliyemrithi alikuwa si mwanawe, si mjukuu wake bali kitukuu wake Louis XV. Haifai!

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Kenya isilale kufufua uchumi

Arsenal waponea chupuchupu kulazwa na Leeds United baada ya...