Akili MaliMakala

Omena inavyotumika kuunda vitafunwa maridadi

Na SAMMY WAWERU October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

OMENA ni mojawapo ya spishi za samaki ambao hushabikiwa sana eneo la Nyanza. 

Wanavuliwa kutoka Ziwa Victoria, upande wa Kenya na Uganda.

Samaki hawa wanaofahamika kwa Kiswahili kama dagaa, wamesheheni virutubisho kama vile Protini, mafuta, mafuta ya omega-3 na madini ya Calcium.

Aghalabu, ni kitoweo kinachoandamanishwa na ugali, mboga au kachumbari.

Licha ya tija zake anuwai kiafya, omena hazina mashabiki wengi vile nchini kwa sababu ya harufu yake hasa zisipopikwa vizuri.

Omena zilizopakiwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Kwa kiasi kikubwa, samaki hawa wadogo wanatumika kama mojawapo ya malighafi kuunda chakula cha mifugo.

Aidha, wanachukuliwa kama chakula cha watu maskini.

Dhana hiyo hivi karibuni huenda ikawa historia kufuatia mradi unaoendelezwa na Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Unalenga kuhamasisha ulaji wa dagaa, kwa kuunda vitafunwa – snaki kwa kuzichakata na bidhaa zingine.

“Tunalenga kuhamasisha ulaji wa omena kwa kuzichakata snaki, ili kuondoa dhana yake potovu,” anasema Prof Nelson Ojijo kutoka kitengo cha Masuala ya Sayansi ya Teknolojia JKUAT.

Prof Nelson Ojijo kutoka kitengo cha Masuala ya Sayansi ya Teknolojia JKUAT akielezea kuhusu uchakataji wa omena ili kuhamasisha ulaji wa samaki hao wadogo. PICHA|SAMMY WAWERU

Mradi huo unaendeshwa chini ya programu inayojulikana kama Strengthening Agricultural Knowledge and Innovation Ecosystem for Inclusive Rural Transformation and Livelihoods in Eastern Africa (AIRTEA), na Prof Ojijo ni kati ya Wanasayansi wanaouongoza.

Ukiwa ulizinduliwa 2022, mradi huo wa miaka miwili na nusu unafadhiliwa na muungano wa Bara Uropa (EU), kwa ushirikiano na shirika la

United States Agency for International Development (USAID).

Mtandao huo wa usindikaji ambao Prof Ojijo anasema umefanikishwa baada ya JKUAT 2021 kuomba ufadhili kutoka kwa EU, anaamini ukikumbatiwa kikamilifu utasaidia kuboresha ulaji wa omena Kenya na kupiga jeki wavuvi.

Taasisi hiyo guru katika masuala ya utafiti wa kilimo na teknolojia, inaongeza dagaa thamani kwa kuzichanganya na mseto wa unga wa nafaka.

Vitafunwa vilivyochakatwa kwa kutumia omena na unga wa nafaka. PICHA|SAMMY WAWERU

“EU ilitupa ufadhili wa Sh35.4 milioni (thamani ya Kenya), nayo USAID ikatuongezea Sh58 milioni,” akafichua Prof Ojijo wakati wa mahojiano na Akilimali Dijitali JKUAT.

AIRTEA inatekelezwa na Jukwaa la Kutafiti Masuala ya Kilimo Barani Afrika, Muungano wa Kupigajeki Utafiti wa Kilimo Afrika Mashariki na Kati, na Shirikisho la Wakulima Afrika Mashariki.

Kwa kutumia unga wa mahindi, wimbi, ngano au mihogo, huchanganya na omena kuunda vitafunio, snaki zenye muundo unaofanana na spaghetti (noodle), dagaa zilizokaushwa na zingine kukaangwa kwa mafuta.

Kulingana na Prof Ojijo, hutumia mashine maalum inayojulikana kama extruder.

Vilevile, kisiagi (posho mill) na ile ya kuchanganya unga, pia zinatumika katika shughuli hiyo.

Mtambo wa kuongeza omena thamani JKUAT, ukichakata samaki hao wadogo. PICHA|SAMMY WAWERU

“Zinapochakatwa, tunahakikisha harufu isiyopendwa na wengi inapungua au inaondoka kabisa na kufanya snaki ziwe na mvuto,” anaelezea, akisisitiza umuhimu wa rangi kurembesha vitafunio hivyo na kuzifanya zitoe sauti kama ya kripsi zinapotafunwa.

Hali kadhalika, hutiwa sukari ili kuongeza ladha, mtafiti huyo akiarifu kwamba mradi huo unapania kuhamasisha ulaji wa dagaa hasa miongoni mwa vijana na watoto kuboresha afya.

Hutoa omena kutoka Bichi za Dunga, Gatuzi la Kisumu na Maringa (Busia), ambapo kupitia mradi huo wavuvi pia hufunzwa uchakataji wake.

Isitoshe, wanaelimishwa haja ya kudumisha hadhi ya usafi.

Mpango huo, hali kadhalika, unalenga kuimarisha jinsi wavuvi hukausha omena kila bichi ikinufaika kwa kutengenezewa kituo cha kisasa kwa minajili ya shughuli hiyo ambacho Prof Ojijo anasema kimepunguza saa za kukausha kutoka nane hadi mbili.

Kiwango kikubwa cha wavuvi hutegemea mifumo ya zamani, Mwanasayansi huyo akidokeza kwamba AIRTEA inatazamia kuunda vituo vingine zaidi.

Vitafunwa vya rangi vilivyoundwa na JKUAT kwa kutumia omena na unga wa mahindi. PICHA|SAMMY WAWERU

Omena inawakilisha asilimia 40 ya samaki wanaovuliwa Ziwa Victoria, na Prof Ojijo anasikitika kwamba wavuvi hupoteza zaidi ya asilimia 50 ya bidhaa hiyo kwa sababu ya ukosefu wa miundomsingi bora kuzikausha na kuhifadhi, hususan msimu wa mvua – jua likikosa kuangaza miale yake vizuri.

“Kwa sasa, mashine tunayotumia inasindika kilo 25 (unga uliochanganywa na omena) kwa kila saa – kiwango hiki kikitoa pakiti 800 hadi 1, 000 za gramu 100 kila moja,” Prof Ojijo anafafanua.

Kiwango hicho cha uzalishaji kinaweza kuongezeka mara dufu wakipata mitambo ya kibiashara, JKUAT ikiomba wadhamini kujitolea kushirikiana nao.

Uchakataji inaoendeleza ni wa kutafiti tu, na wanatumia mashine ya extruder ya maabara.

Bichi ya Dunga huzalisha kilo 13, 000 za omena kila mwezi, na Marenga, Busia, kilo 160, 000.

Kila bichi husambazia JKUAT kilo 25 za omena kila mwezi, Prof Ojijo akiamini wakigeuza utafiti huo kuwa biashara wavuvi watapata afueni na kuwaondoa kinywani mwa mabroka.

Mfanyakazi kutoka JKUAT wakati wa maonyesho ya ASK Nairobi 2024 akionyesha snaki za omena zilizorembeshwa kwa rangi. PICHA|SAMMY WAWERU

Kuhusu mauzo, alisema 2024 walifanya majaribio wakati wa maonyesho ya kilimo yanayoandaliwa na ASK kila mwaka, pakiti ya gramu 100 ikinunuliwa mithili ya mahamri moto kwa Sh100 pekee.

Majaribio hayo walifanya katika ASK Nyeri na Nairobi.

Hivi karibuni, anatazamia bidhaa za omena wanazounda zitaingia sokoni, baada ya kuidhinishwa na Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs).