ONGAJI: Serikali ijitolee kikamilifu kuwalinda raia walioko mataifa ya kigeni
Na PAULINE ONGAJI
HIVI majuzi shirika la habari la kimataifa la CNN lilichapisha makala yaliyoonyesha wanawake wa Kenya walivyokuwa wakilalama kuhusu dhuluma walizokuwa wakikumbana nazo katika ubalozi wa Kenya jijini Beirut, Lebanon.
Ni suala lililoisukuma serikali kuahidi kutuma maafisa wake jijini Beirut kupeleleza taarifa za dhuluma dhidi ya wanawake Wakenya wanaotafuta usaidizi katika ubalozi wa Kenya nchini humo.
Japo ukweli wa madai haya haujabainika, visa vya aina hii ni ishara tosha ya mateso wanayopitia wasichana na wanawake wa humu nchini wanaojituma kwenda kutafuta ajira Mashariki ya Kati.
Nakumbuka makala fulani ya shirika la habari la Thomson Reuters Foundation kuhusu mjakazi kutoka Kenya nchini Lebanon aliyemwagiwa dawa ya kuondoa madoa kama adhabu ya kutofanya kazi upesi.
Kumekuwa na visa vya wanawake wa humu nchini wanaosaka ajira katika maeneo hayo, kudhulumiwa kingono na mambo yakiwa mabaya zaidi, kurejeshwa nchini wakiwa katika majeneza.
Ni visa ambavyo wakati mmoja vilisababisha serikali ya Kenya kupiga marufuku raia wake kusaka ajira hasa ya nyumbani katika maeneo haya, na kutupilia mbali leseni za zaidi ya mashirika 900 yanayopeleka wafanyakazi huko.
Lakini je ni uhalisi kupambana na tatizo hili kwa njia hii?
Wengi wa wasichana na wanawake hawa hutoka katika familia zilizosakamwa na ufukara ambapo kwao afadhali kuhatarisha maisha yao ili kujaribu kupata riziki. Kumbuka kuwa wengi hupelekwa huko kwa ahadi ya kupata ajira ya mashahara mzuri na kuepuka janga la ukosefu wa ajira linalokumba mamia ya maelfu ya Wakenya.
Haya yakijiri, ni hatua zipi ambazo serikali imechukua kuhakikisha kwamba wanaofanyiwa unyama huu wanachukuliwa hatua?
Sijakumbana na kisa chochote ambapo serikali imetoa msimamo mkali dhidi ya nchi husika kuhakikisha kwamba wanaotekeleza unyama wa aina hii dhidi ya raia wake wanachukuliwa hatua.
Na je ni wakati upi ambapo umesikia mwili wa muathiriwa umefanyiwa uchunguzi kubaini kiini cha kifo badala ya kuunga mkono kipumbavu sababu zinazotolewa huko walikotoka?
Je umewahi sikia serikali kupitia taasisi husika ikifuatilia visa hivi kuhakikisha kwamba wanaokuja pasipo kupewa mshahara wamepewa?
Kuna hatua zipi ambazo zimechukuliwa kuhakikisha kwamba familia zinazoachwa angalau zimesaidiwa kifedha baada ya kupoteza mpendwa kwa njia hii?
Vitisho pekee havitatosha kuwazuia wasichana wetu kuenda katika mataifa hayo ya utumwa. Aidha, vita hivi vitasalia kuwa mtihani mgumu hasa ikizingatiwa kwamba bado wasichana wengi wako radhi kusafiri hadi nchi hizi, licha ya kufahamu vyema kuhusu hatari inayowakodolea macho pindi wanapofika huko.
Itakuwa vigumu kukabiliana na tatizo hili huku katika nchi maskini kama Kenya ambapo vijana wameendelea kugubikwa na wingu la umaskini kutokana na ukosefu wa ajira.
Kumbuka kwamba kulingana na Benki ya Dunia, nchini Kenya, ni asilimia sita pekee ya Wakenya wanaoingia katika sekta ya ajira nchini, wanaopata ajira rasmi.