• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
ONYANGO: BBI: Uhuru, Raila wasikilize rai za wakosoaji

ONYANGO: BBI: Uhuru, Raila wasikilize rai za wakosoaji

Na LEONARD ONYANGO

MSIMAMO wa viongozi wanaounga mkono mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kwamba mlango wa kuufanyia marekebisho tayari umefungwa, unafaa kushutumiwa vikali.

Viongozi hao wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, walipokutana mjini Naivasha mapema wiki hii, walishikilia kuwa sasa wataanza mchakato wa kuupigia debe mswada wa BBI jinsi ulivyo.

Waungaji wa BBI wamekuwa wakijipiga vifua katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa wako tayari kukutana debeni na wanaopinga mswada huo wakati wa kura ya maamuzi mwaka ujao.

Majigambo hayo yanaweza kufasiriwa kwamba wafadhili wa BBI wana njama fiche ndani ya mswada huo na wala si kuunganisha Wakenya.

Taasisi na wataalamu mbalimbali wamekuwa wakikosoa baadhi ya vifungu ndani ya mswada wa BBI unaolenga kurekebisha Katiba.

Kwa mfano, Baraza la Wanasheria la Kimataifa (ICJ) limeonya kuwa Idara ya Mahakama huenda ikadhibitiwa na rais iwapo mswada wa BBI utapitishwa jinsi ulivyo.

Mswada wa BBI unapendekeza kuwa rais awe akiteua maafisa wa mamlaka ya kuchunguza maadili ya mahakimu, majaji na maafisa wengineo wa Idara ya Mahakama.

ICJ inasema kuwa rais hafai kupewa mamlaka ya kuteua maafisa hao ili kulinda uhuru wa Idara ya Mahakama. Iwapo mswada huo utapitishwa jinsi ulivyo, rais huenda akatumia vibaya mamlaka yake na kugandamiza majaji na mahakimu wanaotoa uamuzi unaokinzana na matakwa ya serikali.

Naye Naibu wa Rais William Ruto amekuwa akisisitiza kuwa kuna haja ya kufanya mazungumzo ili kulainisha masuala tata yaliyo ndani ya mswada wa BBI. Moja ya masuala ya ambayo Naibu wa Rais anahitaji yabadilishwe ni pendekezo kwamba makamishna wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wawe wakiteuliwa na vyama vya kisiasa.

Dkt Ruto anasema vyama kuteua makamishna wa IEBC ni sawa na timu ya soka kutoa refarii.

Suala la kuleta mageuzi ndani ya IEBC lisiposhughulikiwa kwa makini huenda tukajuta baadaye; chambilecho wahenga kuwa majuto ni mjukuu, huja baadaye.

Iwapo vyama vitatoa makamishna wa tume ya uchaguzi huenda kukawa na hatari ya kutumbukiza nchi kwenye ghasia. Kila kamishna atavutia upande wa chama chake na hivyo kutatiza shughuli za tume ya uchaguzi na hatimaye kusababisha vurugu nchini.

Ikiwa kweli lengo kuu la BBI ni kuunganisha Wakenya, Rais Kenyatta na Bw Odinga hawana budi kuzingatia kujumuisha mapendekezo ya wakosoaji kwenye mswada wa BBI.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kaunti zitafute mbinu za kujitegemea kifedha

MUTUA: Funzo kuu katika jekejeke la kusubiri matokeo ya...