ONYANGO: Miundomsingi katika shule iboreshwe kabla ya Januari
Na LEONARD ONYANGO
SERIKALI imelaza damu tangu Waziri wa Elimu George Magoha alipotangaza kuwa hakutakuwa na masomo mwaka huu.
Hakuna mikakati yoyote iliyowekwa na serikali kuboresha miundomsingi shuleni ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa salama kutokana na maambukizi ya virusi vya corona shule zitakapofunguliwa mwaka ujao.
Serikali imelaza damu labda kwa kudhani kwamba virusi vya corona vitaisha kufikia Desemba mwaka huu.Katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona; ishara kwamba janga hili halitaisha wakati wowote hivi karibuni.
Hakuna juhudi zozote zinazofanywa na Wizara ya Afya kupunguza kasi ya maambukizi mbali na kuhimiza kila kaunti kuwa na vitanda 300 vya kulaza waathiriwa wa virusi vya corona.
Kufikia sasa, kuna chanjo mbili ambazo zimeonyesha matumaini ya kuokoa ulimwengu kutokana janga la virusi vya corona.
Chanjo ambazo zimeonekana kufaulu katika majaribio ya mwanzoni ni ile iliyotengenezwa na kampuni ya Moderna Therapeutics na ile ya Chuo Kikuu cha Oxford.
Majaribio ya kwanza ya chanjo iliyotengenezwa na Moderna Therapeutics ilihusisha watu 45 na kudhihirisha kuwa iliwasaidia kujikinga na virusi vya corona.
Hata hivyo, baadhi ya washiriki walipatwa na maumivu kidogo ya kichwa baada ya kudungwa chanjo hiyo. Chanjo hiyo inatarajiwa kufanyiwa majaribio ya pili na ya tatu kwa binadamu kabla ya kuidhinishwa kutumika.
Kinga hiyo huenda ikawa tayari Juni au mwishoni mwa 2021.Chanjo inayotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford kwa ushirikiano na AstraZeneca Plc ilionyesha kufaulu baada ya kufanyiwa majaribio ya kwanza kwa watu 1,077.
Chanjo hiyo inawezesha mwili kujilinda dhidi ya virusi vya corona.Hata hivyo, Chuo Kikuu Cha Oxford kinasema kuwa chanjo hiyo itakuwa tayari mwaka ujao iwapo itafaulu katika majaribio ya pili na ya tatu.
Lakini jambo la kukatisha tamaa zaidi ni kwamba, mataifa tajiri zaidi ya 70 yameagiza kinga hiyo mapema.Hiyo inamaanisha kuwa chanjo hiyo itafika nchini Kenya baada ya mataifa hayo kuitumia. Hivyo, kinga hizo huenda zikafika humu nchini mnamo 2022 au 2023.
Iwapo serikali haitaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanarejelea masomo yao kuanzia Januari mwaka ujao, Prof Magoha kwa mara nyingine atalazimika kufulitilia mbali kalenda ya elimu ya 2021.
Serikali inafaa kutumia muda huu ambao wanafunzi wako nyumbani kufanya marekebisho yanayohitajika katika shule zote za umma ili shule zifunguliwe Januari mwaka ujao hata kama maambukizi ya virusi vya corona yatakuwa juu.
Wabunge nao wanapasa kutumia fedha kutoka Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF) kujenga vyumba vya madarasa na kujenga maeneo kadha ambapo wanafunzi wanaweza kunawia mikono.