MakalaSiasa

ONYANGO: Rais akabili ukabila katika utumishi wa umma

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

TUME ya Kuajiri Watumishi wa Umma (PSC) miezi miwili iliyopita ilitoa ripoti iliyoonyesha kuwa sekta ya umma inadhibitiwa na watu kutoka jamii tano tu kati ya kabila 42 zilizopo humu nchini.

Ripoti hiyo ya PSC iliyowasilishwa Bungeni, ilionyesha kuwa watu kutoka jamii ya Wakikuyu, Waluhya, Wakisii, Maasai na Waembu wamechukua asilimia 53 ya nafasi za kazi katika idara mbalimbali za serikali.

Wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo mwenyekiti wa PSC, Bw Stephen Kirogo alikiri kwamba hakuna usawa wa kijamii katika uajiri wa wafanyakazi wa umma.

Aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Uwiano na Utangamano kuwa wameanza mikakati ya kuhakikisha kuwa watu kutoka jamii zote wananufaika na nafasi za kazi kwa usawa.

Mwenyekiti wa PSC alisema miongoni mwa mikakati ambayo tume hiyo imeweka, ni kuhakikisha usawa katika uajiri wa vijana 3,600 ambao watapewa mafunzo ya nyanjani katika idara mbalimbali za serikali wanatoka katika jamii zote 44.

Ni lini tume ya PSC ilibaini kwamba hakuna usawa wa kikabila miongoni mwa watumishi wa serikali? Ikiwa ilifahamu hilo zamani, mbona inatuhadaa kwamba imeanza kuchukua hatua ya kuhakikisha usawa sasa?

Ripoti kuhusu ukosefu wa usawa wa kijamii miongoni mwa watumishi wa umma zimekuwa zikitolewa mara kwa mara.

Mnamo 2013, ripoti ya Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ilifichua kuwa kaunti 34 kati ya 47 zimeajiri watu kutoka jamii moja kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo pia ilifichua kuwa asilimia 80 ya kazi katika mashirika ya umma zilitwaliwa na watu kutoka jamii sita; Wakikuyu, Wakalenjin, Wakamba, Wajaluo, Wakisii na Waluhya.

Kwa mfano, ripoti ilifichua kuwa asilimia 24 ya wafanyakazi walioajiriwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) wanatoka jamii ya Wakikuyu.

Ripoti kuhusu wafanyakazi katika vyuo vikuu iliyotolewa na NCIC mnamo 2016 pia ilibaini kwamba ukabila umekolea katika taasisi hizo za elimu ya juu.

Kila mara ripoti hizo zinapotolewa, tume ya NCIC hutoa ahadi hewa kwamba itaalika Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) ichunguze uajiri wa wafanyakazi katika idara za serikali.

Ukweli ni kwamba ukabila katika ajira serikalini unasababishwa na utamaduni ambao umekita mizizi nchini kwamba ili kupata kazi ni sharti ujuane na mtu serikalini. Ufisadi na siasa chafu pia vimemechangia kwa kiasi kikubwa.

Ikiwa kweli Rais Uhuru Kenyatta anataka kuangamiza ufisadi nchini hana budi kuhakikisha kuwa kila Mkenya – maskini au tajiri, anajuana na wakubwa au la, anatoka kabila kubwa au dogo – anapata nafasi ya kuajiriwa kwa kuzingatia kuhitimu kwake.

Iwapo upendeleo utaendelea katika ajira basi hata ripoti ya jopo lililokuwa likikusanya maoni kuhusu namna ya kuunganisha Wakenya itakuwa bure.