Makala

ONYANGO: Serikali yacheza na maisha ya Wakenya kuhusu coronavirus

February 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya serikali ya Kenya kuruhusu kurejelewa kwa safari za ndege kutoka China hadi humu nchini inafaa kukemewa na Wakenya.

Safari hizo huenda zikatoa mwanya kwa virusi vya homa ya Corona ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,700 nchini China kusambaa na kuingia humu nchini.

Kulingana na ubalozi wa China humu nchini, ndege ya China Southern Airlines imerejelea safari zake kutoka eneo la Guangzhou hadi Nairobi na sasa itakuwa inakuja humu nchini mara moja kwa wiki.

Ndege hiyo ilitua humu nchini Jumatano huku wizara ya Afya ikisema kwamba abiria wote 239 waliotoka China walipimwa kabla ya kuondoka na pia walipokuwa ndani ya ndege na kuthibitishwa kuwa hawakuwa na virusi vya Corona.

Ikizingatiwa kwamba virusi vya Corona huchukua takribani siku 14 kujitokeza hivyo basi vipimo hivyo si vya kuaminiwa.

Jiji la Guangzhou ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na virusi vya Corona nchini China. Benki Kuu ya China tawi la Guangzhou hata imekuwa ikiharibu fedha zilizotoka hospitalini, masoko ya vyakula na usafiri wa umma kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya virusi ya ugonjwa huo hatari.

Kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Corona kilichothibitishwa nchini Australia mnamo Januari 25, mwaka huu, kilikuwa cha abiria wa kiume aliyekuwa ametoka jijini Guangzhou, China.

Watu zaidi ya 360 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona jijini Guangzhou na wengine takribani 10 wamethibitishwa kufariki.

Marufuku

Mataifa zaidi ya 30, yakiwemo yaliyostawi kiuchumi, yamepiga marufuku safari za ndege kutoka China; lakini Kenya inaonekana kutojali. Haijali. Wageni kutoka mataifa yaliyothibitisha visa vya homa ya Corona wanaendelea kuingia humu nchini kiholela.

Kwa mfano, Iraq imepiga marufuku safari za ndege katika mataifa tisa ambayo yamethibitishwa kuwa na idadi ya juu ya waathiriwa wa virusi vya Corona. Iraq imepiga marufuku ndege zote kutoka China, Iran, Japan, Kore Kusini, Thailand, Singapore, Italia, Bahrain na Kuwait.

Ireland imefutilia mbali mashindano ya mchezo wa raga baina yake na Italia ambayo imethibitisha kuwa na waathiriwa zaidi ya 450 wa homa ya Corona.

Nchi ya Misri pia imesimamisha safari za ndege yake, Egyptair, kuelekea nchini China kwa muda usiojulikana.

Lakini humu nchini, wizara ya Afya inaonekana kuachia ubalozi wa China humu nchini kutufanyia maamuzi kuhusu namna ya kukabiliana na maradhi hayo.

Wiki mbili zilizopita ubalozi wa China ulitangaza kuwa raia wake wanaoingia humu nchini watatakiwa kujitenga wenyewe kwa siku 14 kabla ya kutangamana na watu wengine.

Wakenya walitarajia wizara ya Afya ipuuzilie mbali pendekezo hilo la ubalozi wa China, lakini ikasalia kimya. Hiyo ni ithibati kwamba Kenya haijajiandaa kukabiliana na homa ya Corona na maisha ya Wakenya yako hatarini.