• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
ONYANGO:  Sura ya 6 ya katiba kuhusu maadili haina maana, iondolewe

ONYANGO: Sura ya 6 ya katiba kuhusu maadili haina maana, iondolewe

Na LEONARD ONYANGO

KATIBA ya Kenya ilipopitishwa mnamo 2010 ilimiminiwa sifa tele huku ikitajwa kuwa bora zaidi barani Afrika na miongoni mwa zile zilizo bora zaidi duniani.

Hii ni kwa sababu ilisheheni sura zilizoangazia maslahi ya vijana, wanawake, walemavu na makundi mengineyo yaliyoonekana kutengwa.

Katiba pia iliangazia kwa kina maadili, uadilifu, demokrasia, utawala bora na usawa katika ugavi sawa wa rasilimali za nchi.

Lakini katiba hiyo sasa inaonekana kutekwa nyara na wanasiasa na mengi ya mambo yaliyoandikwa ndani yake hayajatekelezwa.

Miongoni mwa sehemu katika katiba zinazoonekana kutokuwa na kazi ni Sura ya Sita inayohusu maadili ya viongozi wanaoshikilia afisi za umma.

Kuhusu uwajibikaji wa viongozi, kifungu cha 73 cha Sura ya Sita ya Katiba kinasema kwamba kiongozi anafaa kuheshimu watu, kuletea nchi heshima, kuwa mwaminifu, kuweka kando masilahi ya kibinafsi katika utekelezaji wa majukumu yake na kuwa na nidhamu.

Kifungu cha 75 kuhusu maadili, kinasema kiongozi anayedunisha afisi anayoshikilia kutokana na mienendo yake mibovu atatimuliwa kutoka afisini.

Mara ngapi tumeona au kusikia viongozi hasa wanasiasa wakirushiana cheche za matusi?

Kisa cha hivi karibuni ni kile cha Gavana wa Nairobi Mike Sonko alipomtusi Mwakilishi Mwanamke wa Nairobi Esther Passaris.

Mara ngapi tumeona picha au video za aibu za viongozi wetu zikisambazwa mitandaoni?

Ukitathmini kwa makini, utabaini kuwa karibu nusu ya wafanyakazi wa kaunti ni jamaa wa gavana, naibu gavana au mawaziri wa kaunti husika.

Kadhalika, nyingi ya kampuni zilizopewa kandarasi na serikali ya kitaifa au kaunti ni za marafiki au jamaa wa wakuu serikalini.

Tangu kuanza kutekelezwa kwa katiba miaka tisa iliyopita, hakuna kiongozi ambaye ametimuliwa kwa kukiuka Sura ya Sita mbali na aliyekuwa Naibu wa Jaji Mkuu Nancy Baraza aliyeng’olewa afisini kwa kumchuna pua mlinzi mmoja wa duka la jumla.

Sura ya Sita imetekwa nyara na wanasiasa wala haina tena manufaa yoyote kwa Wakenya na inafaa kuondolewa katika Katiba.

Sura ya Sita sasa inatumiwa kugandamiza vijana wanaosaka kazi kwa kuwataka kuwasilisha marundo ya stakabadhi kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuoni (HELB), Mamlaka ya Ushuru (KRA), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), na kadhalika wanapotafuta kazi katika afisi za umma.

You can share this post!

MUTANU: Wazazi wasipowaelekeza watoto, upotovu utazidi

NGUGI: Viongozi wawe mfano bora maana wengi huwafuata

adminleo