Makala

ONYANGO: Uhasama kati ya Kabila na Tshisekedi uwe funzo kwa Raila

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka hivi majuzi alikuwa nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) katika juhudi za kupatanisha Rais Felix Tshisekedi na Rais (Mstaafu) Joseph Kabila.

Uhasama baina ya wawili hao umekuwa ukitokota kwa miezi miwili sasa baada ya Tshisekedi kushikilia kuwa atavunja mkataba ambao alitia saini kwa siri kabla ya kukabidhiwa mamlaka ya nchi hiyo na Kabila Januari, mwaka jana.

Mkataba huo wa maelewano ulitiwa saini nyumbani kwa Kabila katika eneo la Kingakati jijini Kinshasa na ulishuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta, Rais Abdel Fattah Sisi wa Misri na kiongozi wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Kati ya mambo yaliyokuwa katika mkataba huo wa siri, ni kumtaka Rais Tshisekedi kumlinda Kabila pamoja na familia yake dhidi ya kushtakiwa kwa makosa ya mauaji au ufujaji wa rasilimali za umma.

Kabila pamoja na familia yake pia walifaa kupewa hadhi kubwa nchini DRC. Maelfu ya watu waliuawa kinyama na vikosi vya usalama wakati wa utawala wa Kabila aliyeongoza taifa hilo kati ya 2001 na 2019. Huenda Kabila alihofia kuwa angeshtakiwa baadaye kutokana na mauaji hayo.

Mwaka mmoja na nusu baada ya kutwaa hatamu za uongozi, Rais Tshisekedi ametangaza kupuuzilia mbali mkataba huo huku akisema kuwa sheria ni lazima ifuate mkondo wake.

Tshisekedi amekuwa akisisitiza kuwa yuko tayari kuvunja bunge na kuandaa uchaguzi mpya iwapo hatapata chama cha kufanya muungano nacho kuendesha serikali.

Chama kinachodhibitiwa na Kabila kina wabunge 300 kati ya 500 walio katika bunge la DRC. Wabunge hao wote 300 wa Kabila walikuwa wakiunga mkono Tshisekedi kabla ya uhusiano wake na Kabila kutumbukia nyongo.

Kabila tayari ameandikia barua Umoja wa Afrika (AU), Marais Kenyatta, Sisi na Ramaphosa akiwataka kuingilia kati na kumshawishi Rais Tshisekedi kuzingatia mkataba waliotia saini.

Kabla ya kutangaza rasmi ushirikiano wao mnamo Machi 2018, Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walifanya ‘mkataba’ wa siri ambao haujawahi kuwekwa wazi.

Mara baada ya kutangaza kushirikiana, Rais Kenyatta na Bw Odinga walianza mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ili kurekebisha Katiba.

Bw Odinga amekuwa katika mstari wa mbele ‘kusukuma’ BBI. Lakini Bw Odinga anafaa kujihadhari asije akaachwa kwenye mataa baada ya kupitishwa kwa mswada wa BBI. Kama wasemavyo Waswahili: mwenzako akinyolewa, chako tia maji. Siasa ni mchezo mchafu uliosheheni usaliti.