Makala

ONYANGO: Wafanyakazi shuleni wanafaa kutibiwa corona bila malipo

November 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

WALIMU wamepata afueni baada ya mwajiri wao kutangaza mapema wiki hii kuwa watapewa matibabu ya bure endapo wataambukizwa virusi vya corona.

Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iliwahakikishia walimu wake zaidi ya 337,000 kuwa itawalipia gharama ya matibabu ya virusi vya corona baada ya Hazina ya Bima ya Afya nchini (NHIF) kusema kuwa haitagharimikia matibabu ya wateja wake wanaopatwa na ugonjwa huo.

Tangazo hilo la NHIF linamaanisha kwamba Wakenya wanaoambukizwa virusi vya corona watajilipia gharama ya matibabu.

Japo tangazo hilo la TSC ni habari njema kwa walimu, serikali inafaa pia kutoa matibabu ya bure kwa wafanyakazi wengine shuleni kama vile walimu wa ziada walioajiriwa na Bodi za Usimamizi wa Shule (BOM), wapishi, walinzi, nakadhalika.

Wafanyakazi hao wa shule wanahatarisha maisha yao kwani wanatangamana na wanafunzi mara kwa mara.

Kutokana na uhaba wa walimu uliopo humu nchini, walimu wa ziada wanaoajiriwa na bodi za BOM wamekuwa wa msaada mkubwa katika kuziba pengo hilo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, kuna zaidi ya walimu 43,000 walioajiriwa na bodi za BOM nchini. Shule zitakapofunguliwa Januari 4, mwaka ujao, walimu wa BOM zaidi watahitajika ili kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule za umma.

Wengi wa wazazi waliathiriwa pakubwa na janga la virusi vya corona na huenda wakahamishia watoto wao katika shule za umma baada ya kulemewa na karo kwenye shule za kibinafsi.

Tangu shule kufungwa ghafla miezi minane iliyopita kufuatia janga la virusi vya corona, walimu hao wa BOM wamekuwa wakihangaika kwani wengi wao hawakulipwa mshahara.

Sawa na wahudumu wa afya, wafanyakazi wa shuleni wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya corona. Tafiti mbalimbali zilizofanywa kote duniani zinaonyesha kuwa watoto hawaathiriwi zaidi na virusi vya corona ikilinganishwa na watu wazima.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Hospitali ya Kitaifa ya Washington DC nchini Amerika, ulibaini kwamba mtoto anapopatwa na virusi vya corona anaweza kuvisambaza kwa karibu wiki moja bila yeye kuwa mgonjwa.

Hivyo, walimu na wafanyakazi wengine wa shule kama vile wapishi wanapotangamana na watoto hao wanakuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya corona.

Katika shule nyingi, walimu walioajiriwa na BOM, wapishi na wafanyakazi wengineo wanalipwa mishahara duni ambayo haiwezi kuwatosheleza kugharimikia matibabu yao wenyewe wanapopatwa na virusi vya corona.

Serikali, kupitia NHIF inafaa kuwapa matibabu ya bure wafanyakazi hao wa shuleni.