ONYANGO: Wanasiasa wamesaliti Katiba kuwaacha raia na njaa
Na LEONARD ONYANGO
BAA la njaa nchini limesalia donda ndugu tangu Kenya ipate uhuru wake zaidi ya nusu karne iliyopita.
Wengi walidhani kwamba, kupitishwa kwa katiba mpya mnamo 2010 kungesaidia kumaliza njaa ambayo imekuwa ikihangaisha mamilioni ya Wakenya kila mwaka, lakini hali haijabadilika miaka kumi baadaye.
Mwaka huu, kwa mfano, ripoti iliyotolewa na shirika la utafiti la Uingereza, mwezi uliopita, inaonyesha kuwa, watu 3.6 milioni watakumbwa na baa la njaa nchini kufikia mwishoni mwa mwaka huu na mwanzoni mwa 2021.
Nzige waliovamia Kenya kuanzia Machi, mwaka huu na janga la virusi vya corona ambalo limetatiza shughuli za kilimo huenda likasababisha idadi kubwa zaidi ya Wakenya kukosa chakula.
Hali hii ingeepukika iwapo Katiba ya 2010 ingetekelezwa kikamilifu katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita. Kifungu cha 43 cha Katiba ya 2010 kinasema kuwa, kila Mkenya ana haki ya kutokeketwa na makali ya njaa. Kila Mkenya ana haki ya kupata chakula bora na cha kutosha.
Kifungu hicho kina maana kuwa, hufai kupigia makofi wanasiasa wanapokuletea msaada wa ‘gorogoro’ moja ya mahindi. Chakula bora na cha kutosha ni haki yako ya kikatiba. Kifungu hiki hakimaanishi kwamba, serikali inafaa kuwapa chakula wananchi ilhali wao wamelaza damu. La hasha. Katiba inamaanisha serikali inafaa kuweka miundomsingi na kuwezesha wakulima kupata pembejeo zinazohitajika kuzalisha chakula cha kutosha.
Lakini wakati wa ukame au janga ambapo watu hawawezi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji wa chakula au kukosa fedha za kununua chakula, serikali ni sharti iingilie kati kwa kuwapa msaada wa kutosha wa chakula wala si ‘gorogoro’ moja. Ripoti iliyotolewa hivi majuzi na shirika la Amnesty International Kenya inaonyesha kuwa, asilimia 40 ya Wakenya hawajui yaliyomo kwenye Katiba ya 2010. Labda hiyo ndiyo sababu Wakenya hawajajitokeza kushinikiza serikali kuwapa chakula wakati wa baa la njaa. Sio kwamba, wasiojua yaliyomo kwenye katiba si wasomi bali wanasiasa ndio wa kulaumiwa.
Wanasiasa wamekuwa wakipigia debe mambo machache tu yaliyomo kwenye katiba ya kuwafaa wao na kutegea mgongo mambo muhimu yanayohusu mwananchi wa kawaida kama vile chakula. Sera ya serikali ya 2012 inayolenga kuhakikisha kuwakila Mkenya anapata chakula cha kutosha haijatekelezwa miaka minane baadaye. Shughuli za kilimo zimegatuliwa, lakini hakuna kaunti iliyo na sera au mwongozo mwafaka wa kuwalinda wakazi dhidi ya makali ya njaa.