Paka 600 kutumika kupambana na panya Kaunti ya Nairobi
MIAKA mitano tangu shirika la Nairobi Feline Sanctuary kuazisha mpango wa kuokoa paka na kuwapa makao, sasa shirika hilo linapania kuanzisha mpango wa kuwapeleka paka hao katika maeneo yalio na panya Kaunti ya Nairobi ili kuwashughulikia.
Mwazilishi wa kutetea haki za wanyama haswa paka Bi Racheal Kibue, alisema kuwa licha ya paka hao kupuuzwa, watatumika kupunguza panya wanaosumbua watu mjini.
“Kuna maeneo mengi hapa nchini ambapo kuna panya wengi. Hivi karibuni tutaanza kuwapeleka maeneo yaliyo na panya ili kuwaangamiza. Paka ambao watasafarishwa katika maeneo hayo, ni wale ambao wanapenda binadamu,” alisema Bi Kibue.
Alisema kuwa baada ya paka hao kukabiliana na panya katika mitaa zilizo na panya wengi, baadaye watakuwa wanachukuliwa na kurejeshwa katika makao yao rasmi.
Kulingana na Bi Kibue, paka hao wana tabia zinazofanana na za wanadamu. Mmoja wao ana njia ya kipekee ya kujibu anapoitwa, baadhi ni walafi huku wengine wakipenda wageni kwa dhati.
“Kila paka hapa ana jina, unapomuita huitika kwa njia mbalimbali. Pia, huonyesha upendo wao kwa binadamu haswa kwa wale huja hapa nyumbani,” alisema Bi Kibue.
Mama huyo wa watoto watano alisema kuwa kwa sasa Kaunti ya Nairobi ina afueni kwa kuokoa paka hao ambao kwa wakati mwingi walipatikana kwenye sehemu zisizohitajika kama vile mikahawa.
“Kila wakati nilikuwa nikipokea simu kutoka kwa wasimamizi wa mikahawa wakisema kuwa kuna paka wanaowasumbua. Nilijukumika kwenda kuwachukua. Pia, kuna wale ambao hutupwa kwenye vichaka na wale ambao wana majeraha,” aliongeza Bi Kibue.
Bi Kibue alianza kuwapa paka hao makao kuanzia mwaka wa 2020 baada ya kutambua kuwa mnyama huyo ananyimwa haki yake, haswa anavyohitaji kuishi na kula.
Haki hiyo ikitokana na mafunzo aliyopata akiwa nchi ya India alipokuwa akipata mafunzo ya mazoezi ya viungo na kudhibiti pumzi (yoga).
Baada ya kurejea nchini Kenya alianza kuokoa paka hao kutoka mitaa mbalimbali jijini Nairobi na kuwapa hifadhi kwenye nyumba yake.
“Paka hapendi kuishi na wanawe. Wakazi wengi walikuwa wakiwaweka kwenye boksi nami nawaokota,” alifafanua.
Kutokana na mapenzi ya kuokoa paka hao, Bi Kibue alihama kutoka nyumba yake yenye vyumba vinne na kwenda kuishi kwingine ili kuwaachia kuwa na makao mazuri.
Kwenye boma hilo, Bi Kibue akilazimika kuwaajiri wafanyakazi watatu ambao huhakikisha paka hao wanapata chakula kila siku na kuishi kwenye mazingira safi.
“Nilikuwa nikiishi hapa lakini kutokana na idadi kubwa ya paka hao, niliondoka kwenda kwingine lakini si mbali na hapa,” alibainisha.
“Wafanyakazi huishi hapa kuhakikisha blanketi zinazotumiwa na paka hao zinaoshwa na kubadilishwa kila siku,” alieleza mama huyo.
Hata hivyo, mama huyo alisema kuwa aliwachanja paka hao na kuwafunga wasizae. Alisema paka mmoja anaweza kuzaa watoto 48 kwa mwaka, hivyo kuna umuhimu wa kudhibiti idadi yao kwenye hifadhi hiyo.
“Tunasimamisha uzalishaji kwa sababu kuna paka wengi wanaoishi katika hali mbaya. Kulisha paka hao, pia ni changamoto licha ya michango inayotolewa mara kwa mara katika kituo hicho,” alifanunua.
Mhifadhi huyo alisema chakula ambacho paka hao hutumia hutoka kwa kampuni huhifadhi nyama na kusafirisha nje ya nchi. Kila siku akigharamia Sh3,500 kwa chakula ya paka hao.
“Wakati mwingine sio kila nyama hupata fursa ya kusarishwa na hivyo huwa afueni kwetu. Kila siku wanahitaji kula nyama ambao tunapata kwa gharama ya chini.”
Alisema kuwa kuna wale paka ambao huchukulia kwa Sh3,000, pesa hizo zikitumika kutibu wanaosalia.