• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Pakchong – Nyasi yenye virutubisho tele kwa mifugo

Pakchong – Nyasi yenye virutubisho tele kwa mifugo

NA SAMMY WAWERU

HUKU gharama ya chakula cha mifugo cha madukani ikizidi kupanda bei, wakulima wanahimizwa kusaka mbinu mbadala kuipunguza.

Mbali na kuwa na akiba ya kutosha ya nyasi, Joseph Kamau ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mifugo na mfugaji hodari, anasisitiza haja ya wakulima kukumbatia mifumo ya kujiundia malisho.

Anataja nyasi maalum aina ya Super Napier, almaarufu, Pakchong kama kati ya ambazo wafugaji wanapaswa kukuza.

“Zina manufaa tele kiafya kwa mifugo,” Kamau anasema.

Pakchong ni nyasi zenye asili ya Thailand na Kusini Mashariki mwa Asia.

Aidha, nyasi hizo zinachukua karibu siku 60 (sawa na miezi miwili) kukomaa na kuwa tayari kwa mavuno.

Joseph Kamau akionyesha mojawapo ya malighafi anayotumia kujiundia chakula. Huchanganya na nyasi maalum aina ya Pakchong iliyosagwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Kamau, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kaunti ya Murang’a, anasifia nyasi hizo akisema zimemsaidia kupandisha kiwango cha uzalishaji kutoka lita mbili hadi wastani wa lita kumi kwa siku, kila ng’ombe.

Huku ng’ombe wa maziwa wakitakiwa kula malisho yaliyosheheni Protini, Pakchong inakadiriwa kuwa na asilima 16 hadi 18 ya kirutubisho hicho.

Hicho ni kiwango cha juu mno kikilinganishwa na vyakula vingine vya mifugo.

Hii ina maana kuwa nyasi hizo zinapunguzia mkulima gharama ya ufugaji kwa kiwango kikubwa, ikizingatiwa kuwa malighafi kama vile maharagwe ya soya bei yake haikamatiki.

Kamau ana mashine, chaff cutter, ya kukatakata nyasi (kusaga).

  • Tags

You can share this post!

Msichana aitwa kujiunga na shule ya kitaifa ya wavulana

Mwanadada adaiwa kujitia kitanzi kwa kukosa kazi

T L