Pamba ya kisasa kiboko cha mdudu hatari wa Kiafrika
KWA muda mrefu wakulima wa pamba wamekuwa wakihangaishwa na wadudu waharibifu wa zao hilo.
African Bollworm, amekuwa changamoto sugu kwa wakulima wanaojitolea kuboresha sekta ya pamba Kenya.
Mdudu huyu anatajwa si tu hatari hapa nchini, bali pia ametamba Barani Afrika na mataifa mengine duniani yanayolimwa pamba.
Kenya, pamba inakuzwa eneo la Magharibu, Nyanza, Kati, Bonde la Ufa, Mashariki mwa mchi na sehemu kadha Pwani.
Hata hivyo, kulingana na wataalamu pamba ya kisasa ndiyo kiboko chao kwa African Bollworm.
“Wanaolima pamba asilia, kiwango cha unyunyiziaji dawa dhidi ya wadudu ni zaidi ya mara 12,” anasema Dkt Paul Chege, mtaalamu wa masuala ya pamba kutoka International Service for the Acquisition of Agri-biotech Applications (ISAAA) AfriCenter.
ISAAA AfriCenter, ni kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yanayohamasisha kilimo cha mimea iliyoboreshwa na kuimarishwa Kisayansi – Bayoteknolojia.
Pamba ya kisasa, maarufu kama Biotech cotton (bt cotton), imeboreshwa kibayoteknolojia.
Dkt Chege anasema imeimarishwa Kisayansi kiasi kuwa kiwango cha kupulizia dawa za wadudu kimepunguzwa kutoka 12 hadi chini ya nne.
Kauli ya mdau huyu inapigwa jeki na Derleen Mogire, mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).
“Kinachofanya kiwango cha mavuno ya bt cotton kuongezeka, ni idadi ya pulizi dhidi ya mdudu aina ya African Bollworm kupungua pakubwa,” Derleen anaelezea.
Kinyume na dhana kuwa maumbile ya pamba hii ya kisasa ina hulka za mazao mengi kwa sababu ya chembechembe zake, Dkt Chege anasema imetengenezwa kama pamba nyingine yoyote ile.
“Unapopunguza changamoto zinazozonga mimea, kiwango chake cha uzalishaji kinaongezeka mara dufu,” anasisitiza.
Mbegu za biotech cotton, huagizwa kutoka India kupitia asasi husika ya serikali iliyotwikwa jukumu hilo.
Daniel Magondu ni mmoja wa wakulima wa pamba hii katika Kaunti ya Kirinyaga ambaye husambazia wanazaraa mbegu pindi zinapotua nchini.
“Nilikumbatia pamba ya kisasa ilipoidhinishwa kukuzwa Kenya,” Magondu anasema, akikiri biotech cotton kuwa na mazao ya kuridhisha ikilinganishwa na ile ya asilia.
Amekuwa kwenye kilimo cha pamba kwa zaidi ya miaka 30.
“Kimavuno, kwa sababu ya mpunguo wa athari ekari moja kiwango kimeongezeka kutoka kilo 400 (pamba asilia) hadi zaidi ya tani moja,” Magondu anasema.
Pamba ya kisasa iliidhinishwa kulimwa nchini 2018 baada ya Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bidhaa – National Biosafety Authority (NBA), chini ya Kifungu cha 2 cha Sheria ya 2009 kuhusu usalama wa Kibayolojia, kuridhishwa na utafiti uliofanyika.
Magondu, hata hivyo, anasema biotech cotton huchangamkiwa na wadudu aina caterpillar na aphids.
Kati ya mipamba, mkulima huyu hukuza mbaazi na mahindi.