Pambo

Athari za watoto kutumia Akili Unde

Na BENSON MATHEKA August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDADI kubwa ya vijana wanatumia majukwaa ya Akili Unde (AI) kama Claude au ChatGPT kwa shughuli za kila siku kama kazi za nyumbani, kupata mawazo mapya, au kutafsiri lugha.

Lakini kulingana na ripoti ya 2024 kutoka Common Sense Media, asilimia 18 ya vijana walisema wametumia AI kutafuta ushauri kuhusu tatizo la kibinafsi, asilimia 15 waliitumia kuepuka upweke na asilimia 14 waliitumia kutafuta taarifa za kiafya.

Cha kushangaza ni kwamba ni asilimia 37 tu ya wazazi wa vijana wanaotumia majukwaa ya AI wanaojua kwamba watoto wao wanayatumia kuepuka upweke kulingana na utafiti huo wa Common Sense Media.

Watafiti wanasema kutafuta msaada mtandaoni si jambo jipya, lakini hali inabadilika zaidi kwa matumizi ya mpango wa chatbots kama Claude au ChatGPT badala ya mfumo wa utafutaji.AI ya kijamii (social AI companions) hutengenezwa kukidhi mahitaji ya kijamii na kihisia ya watumiaji – iwe ni urafiki, ushauri, au hata mapenzi.

Zinatengenezwa kuonyesha upendo na hukubalika kwa urahisi mambo ambayo vijana hutafuta sana.

“Tunatumia AI kwa sababu tunajihisi wapweke na kwa sababu watu wa kweli ni wakali na wanatuhukumu, lakini AI haifanyi hivyo,” kijana mmoja aliambia watafiti.

Katika hali yenye manufaa, majukwaa haya yangewaandaa vijana kwa mafanikio. Yangehimiza mawasiliano ya kibinadamu, kuweka vizuizi dhidi ya maudhui hatari, kuwaelekeza kwa vyanzo vinavyoaminika, na kueleza wazi kwamba AI si binadamu.

Tathmini ya kina kutoka Common Sense Media iligundua kuwa majukwaa maarufu ya AI hayatimizi viwango vya msingi vya usalama, uwazi, na ulinzi.Masuala muhimu yaliyogunduliwa ni pamoja na, ukosefu wa hatua madhubuti za usalama, taarifa hatari na ushauri usiofaa, kuigiza ngono na mawasiliano hatari ya kingono na maudhui yenye ubaguzi wa kijinsia au wa rangi.Kutokana na hayo, Common Sense Media ilikadiria kiwango cha hatari ya AI kwa watoto ni hasi.

Kwao, faida za majukwaa haya haziwezi kuzidi madhara yake.Wataalam wanasisitiza kuwa hadi pale kampuni zitakapozingatia afya na ustawi wa vijana, ni busara wazazi wachukue tahadhari kubwa. Dkt Nina Vasan, mwanzilishi wa Stanford Brainstorm, anasema bila ulinzi madhubuti, watoto hawapaswi kutumia majukwaa ya AI.

”Karibu nusu ya wazazi katika utafiti wa Common Sense Media, walisema hawajawahi kuzungumza na watoto wao kuhusu AI. Kuzuia ufikiaji hakumaanishi kupuuza sababu zinazowafanya watoto kugeukia AI.