Pambo

Chukua muda kabla ya kumpa mtu moyo wako

Na BENSON MATHEKA August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mapenzi ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu, lakini si kila uhusiano wa kimapenzi huwa wa furaha na ustawi.

Wengi wameingia katika mahusiano kwa sababu zisizo sahihi au bila maarifa ya kutosha, na kuishia kuumia kihisia, kiakili na hata kimwili.

Hisia za upweke au kumbukumbu za zamani hazipaswi kuwa sababu ya kupenda mtu au kurudia mtu aliyeumiza moyo wako. Kuna sababu inayopelekea uhusiano kuvunjika na watu wengi hufanya makosa kurudiana na mpenzi wa zamani.  Hii ni sawa na  kurudia makosa ya zamani.

“Ikiwa familia ya mpenzi wako haikupokei vizuri, hasa ikiwa karibu asilimia 70 wanakukataa, elewa kuna hatari. Familia ni msingi wa ndoa, na kukosa uungwaji mkono kunaweza kusababisha migogoro isiyokwisha. Penzi bila baraka mara nyingi huisha kwa maumivu,” asema mtaalam wa masuala ya mahusiano Ken Kalii.

Watu wengi, asema, huingia kwenye mahusiano kwa sababu ya mvuto wa kimwili bila kuwa na hakika na wanachotaka.  “Ni muhimu kuwa na hakika na unachotaka unapoingia katika uhusiano. Je, unatafuta mtu wa kuwa naye maishani au mtu wa kushiriki uroda? Uhusiano wa muda mrefu usio na msingi wa upendo wa kweli huwa haudumu,” aelezea.

Wataalamu wa mahusiano ya mapenzi wanasema kuingia katika uhusiano kwa sababu tu unahisi mpweke ni kujitakia matatizo. Mapenzi hayawezi kuwa dawa ya upweke. Badala yake, yatakuletea maumivu zaidi mara yanapovunjika, kwa sababu ya kukosa msingi mwingine wa kuyakita, asema Kalii.

Kabla ya ndoa, asema mwanasaikolojia Jane Muthoni, ni muhimu kuweka mipaka. “Sio kila mtu anayeonyesha mapenzi anastahili kujua kila siri yako au uwezo wako maishani. Wengine wanaweza kutumia habari zako kwa njia mbaya endapo uhusiano wako nao utaisha kwa ubaya,” ashauri Muthoni. Hii, asema imewafanya watu wengi kulia kwa majuto.

“Kabla ya kupenda mtu, aeleza Muthoni, jipende wewe kwanza. “Mahusiano yasikuzuie kufuata ndoto zako au kujijenga binafsi. Wale unaowapenda wanaweza kukuacha, lakini huwezi kujiacha. Kamwe usipoteze ndoto zako kwa sababu ya kumfurahisha mtu mwingine,” asema.

Anaonya watu kutomeza chambo haraka. “Uhusiano unaoanza kwa haraka sana mara nyingi hujengwa kwa hisia bandia. Mtu anayekuharakisha kwenye mapenzi anaweza kuwa na ajenda fiche. Usilewe na maneno matamu na zawadi, chukua muda kumjua mtu kabla ya kumpa moyo wako kabisa,” asema.

Mtu asiyeheshimu maoni yako ni hatari, asema Kalii.

“Kama mtu hakusikilizi, au hathamini maoni yako, huyo si mtu wa kuwa naye. Hii ni dalili ya mwanzo ya unyanyasaji wa kihisia au hata kimwili. Mahusiano yanapaswa kujengwa juu ya heshima na usawa,” asema.

Wataalamu wanasema kwamba mapenzi ya kweli yanahusisha kutoa na kupokea kwa usawa. Ikiwa uko na mtu anayejua tu kuchukua iwe ni pesa, muda na nguvu zako  bila kuchangia chochote, basi huo ni uhusiano bandia. Jiepushe mapema kabla hujadhurika zaidi.

Kulingana na Kalii, uhusiano  mzuri  wa kimapenzi ni unaojengwa kwa msingi imara. “Si kila mtu anayekuja katika maisha yako anafaa kuwa sehemu ya safari yako ya mapenzi,” asema.