Pambo

Dada, usisononeke kurekebisha mwanamume mchepukaji, hautaweza

Na BENSON MATHEKA September 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katika ulimwengu wa mahusiano ya leo, wengi wamejifunza kupitia maumivu ya usaliti, udanganyifu na kukosa heshima katika mapenzi.

Wanawake wanalaumu wanawake wenzao wanaochepuka na waume zao. Lakini ukweli mmoja unadumu: Mwanaume mwaminifu hawezi kupagawishwa na mwanamke mwingine isipokuwa mkewe au mpenzi aliyechagua na aliyemkubali.

Ni jambo la kusikitisha kuona wanawake wakipigana, kutukanana au kujidhalilisha kwa ajili ya mwanaume mmoja ambaye hana msimamo, asiye na heshima, wala uaminifu.

Wataalamu  wa masuala ya mahusiano wanawema hili ni kosa kubwa. Kwa sababu ukweli mchungu ni huu;  mwanamke  hawezi “kumuiba” mwanaume ambaye hajitolei kupatikana. Mwanamume anayeruhusu mwanamke mwingine amkaribie, amteke au amchukue, tayari huwa anatafuta njia ya kutoka.

Kuna usemi maarufu: “Usimlaumu yule aliyemnyakua, mlaumu aliyejiachilia.” Mwanaume mwaminifu ataweka mipaka wazi kwa wanawake wengine. Hatatoa nafasi kwa mtu mwingine isipokuwa mpenzi wake. Ataheshimu hisia zako kama mtu wake, muda wako, na uaminifu wako. Hatakufanya ushindane na mwanamke mwingine kwa nafasi yako.

“Mwanaume wa kweli si yule anayekimbizana na kila sketi anayoiona, bali ni yule anayejua thamani ya mwanamke aliye naye. Ni yule anayejitolea kwa uaminifu, anayejenga mawasiliano ya kweli, na anayejua maana ya kuwa mume au mpenzi wa mtu mmoja,” asema mwanasaikolojia Viviane Kanini.

Anaongeza: “Kwa hivyo, dada zangu, acha kupigana kwa ajili ya mwanaume ambaye hakujali hata kukupigania. Mwanaume anayekupenda hatakuweka kwenye hali ya mashindano, bali atakupa uhakika wa nafasi yako. Ukijikuta unajitetea kila mara kwa sababu ya tabia zake, basi jua kuwa si wewe unayehitaji kubadilika, ni yeye,” asema Kanini.

Deborah Kinyanjui, mtaalamu wa masuala ya mahusiano anashauri wanawake wasiharibu muda kurekebisha mwanamume mchepukaji.

“Kumbuka wewe sio kituo cha kurekebisha tabia ya wanaume wenye tamaa ya wanawake. Mapenzi hayafai kuwa mateso. Kama unampenda, lakini anakudhalilisha, anakusaliti na anakufanya uhisi kama haufai, basi huo si upendo — huo ni uharibifu wa moyo na utu wako,” asema Deborah.

Mwanaume anayejiheshimu, asema, hawezi kuibwa na mwanamke. “Na kama aliweza “kuibwa”, basi hakuwa wako kamwe. Mungu anakuepushia machungu ya maisha na kukuandalia kitu bora zaidi. Amini hivyo, jiheshimu, na usikubali kupigania mtu asiyeona thamani yako,” asisitiza.

Kulingana na Kanini, Mwanaume mwaminifu ni baraka lakini mwanaume wa kila mtu ni mzigo. Acha mzigo uende, ushike baraka zako. Uaminifu hauko kwenye midomo, uko kwenye matendo.