Fahamu mikataba ya kabla ndoa, na umuhimu wake katika ugavi wa mali
SHERIA ya Mali ya Ndoa ya 2013 inatambua rasmi mkataba kabla ya ndoa – prenuptial au prenup kwa Kimombo – nchini Kenya. Hii ni mikataba ambayo wanandoa hukubaliana wenyewe na kwa hiari kuhusu usimamizi wa mali zao, kabla kufunga harusi.
Sheria hii ilianza kutumika Januari 16, 2014 na ilifuta Sheria ya Mali ya Wanawake ya 1882 ambayo haikutoa nafasi kwa prenups.Lengo kuu la sheria hii ni kuweka wazi haki na wajibu wa wanandoa kuhusu mali ya ndoa na masuala yanayohusiana nayo.
Kifungu cha 6 (3) cha sheria hii kinatoa fursa kwa watu wanaotarajia kufunga ndoa kuingia katika makubaliano kabla ya ndoa hiyo ili kubaini haki zao kuhusu mali.
Mikataba ya prenup imeanza kutambuliwa Kenya kama njia bora na nafuu kwa wanandoa kushughulikia masuala ya mali waliyokuwa nayo kabla ya ndoa, iwapo watatengana, kutalikiana au kifo kutokea. Kwanza, prenup ni makubaliano yanayofanywa na wanandoa kabla kufunga ndoa.
Yanaweka bayana udhibiti wa kisheria na kifedha wa mali yao binafsi endapo ndoa itavunjika. Kulingana na masharti ya mkataba, unaweza kuhusisha mali kabla au baada ya ndoa, na kuilinda isiwe sehemu ya mgao kati ya wanandoa watalakiana.
Mkataba huu unachukua nafasi ya kwanza dhidi ya sheria zingine zozote kuhusu ugavi wa mali ya ndoa.Sheria inasema mkataba wa prdenup ni lazima uwe kabla ya ndoa kufungwa.
Hata hivyo, inashauriwa kwamba usitiwe saini karibu mno na tarehe ya harusi ili kuepuka shinikizo lisilo la lazima.Pande zote mbili zinapaswa kupewa muda wa kutosha kuelewa na kukubali masharti katika mkataba.
Kuwiana na sheria ya kawaida, mkataba wa prenup haupaswi kutiwa siaini chini ya siku 21 kabla ya ndoa.Pande zote lazima zikubali kwa hiari na kuelewa kikamilifu maana na athari zake.
Mkataba usiwe wa upande mmoja au kunyima yeyote haki – ugavi wa mali haupaswi kupendelea mmoja wa wanandoa.Kila mmoja anpaswa kufichua mali yote aliyonayo, hata ile anayokusudia kuondoa kama sehemu ya mgao wa mali ya ndoa.
Mkataba wa prenup haupaswi kuathiri majukumu ya malezi ya watoto iwapo wanandoa wamejaliwa watoto.Pia unapaswa kueleza kwa uwazi hatima ya kila mali na deni lililotajwa kwenye makubaliano hayo iwapo kutatokea talaka.
Kulingana na sheria, mkataba wa aina hii hauwezi kukiuka sheria yoyote ya jinai. Kwa mfano, ulaghai wa mmoja au wanandoa wote.