Hakuna ndoa mbinguni, ifurahie duniani
MSEMO kwamba hakuna ndoa mbinguni umeendelea kutajwa sana katika jamii kukumbusha wanandoa kuwa furaha ya ndoa hujengwa hapa duniani, kwa juhudi na makusudi ya wahusika.
Wataalamu wa masuala ya ndoa na familia wanasema ndoa si bahati nasibu wala tukio la kimiujiza, bali ni safari inayohitaji mawasiliano, uvumilivu na maamuzi ya kila siku hapa duniani.
Mshauri wa masuala ya ndoa na familia, Bi Jane Achieng’, anasema wanandoa wengi huingia kwenye ndoa wakiwa na matarajio ya juu yasiyoeleweka na yasiyoweza kutekelezeka.
“Wengine huamini ndoa italeta furaha yenyewe. Ukweli ni kwamba furaha hujengwa. Hakuna ndoa kamilifu, lakini kuna ndoa inayofanyiwa kazi kwa makusudi inawiri,” anasema Bi Achieng’.
Mtaalamu huyu anaongeza kuwa wanandoa wanapaswa kujifunza kuwasiliana kwa uwazi, kusikilizana na kutatua migogoro kabla haijawa mikubwa.
Kwa upande wake, Dkt Daniel Mwangi, mwanasaikolojia wa masuala ya familia, anasema shinikizo za maisha ya kisasa zimeongeza migogoro ya ndoa.
“Changamoto za kiuchumi, kazi nyingi, mitandao ya kijamii na matarajio ya jamii vinaathiri sana mahusiano. Wanandoa wakikosa muda wao kwa wao, mapenzi hupungua,” anasema.
Dkt Mwangi anashauri wanandoa kutenga muda wa makusudi wa kuwa pamoja, hata kama ni mazungumzo mafupi kila siku, ili kuimarisha ukaribu wa kihisia.
Mchungaji Peter Odhiambo, naye anakiri kuwa hata katika misingi ya imani, ndoa huhitaji jitihada.
“Imani hutufundisha kupendana na kuheshimiana, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya maamuzi yetu. Ndoa ni agano la duniani, na lazima tulilinde kwa vitendo,” anasema.
Anaongeza kuwa wanandoa wanapaswa kujifunza kusameheana, kwani makosa ni sehemu ya maisha ya kibinadamu.
Wataalamu hawa watatu wanakubaliana kuwa furaha ya ndoa huanza pale wanandoa wanapokubali ukweli kwamba hakuna ndoa isiyo na changamoto.
Badala ya kutafuta ukamilifu, wanandoa wanahimizwa kutafuta uelewano na maendeleo ya pamoja. Pia wanashauri wanandoa wasiogope kutafuta ushauri wa kitaalamu wanapokumbana na matatizo.
“Katika jamii ambako talaka zinaongezeka, ujumbe muhimu ni ndoa si mahali pa mateso bali pa furaha. Hata hivyo, furaha hiyo haiwekwi kando kusherehekewa mbinguni, bali hujengwa hapa duniani kwa subira, mawasiliano na upendo wa dhati,” asema Dkt Mwangi.
Katika hafla maalum ya kuadhimisha na kuimarisha ndoa, iliyofanyika Embu mwishoni mwa mwaka jana wanandoa walikumbushwa kuwa upendo si jambo la kubahatisha, bali ni safari inayohitaji kupaliliwa kila siku hapa duniani.
Wanandoa walikumbushwa kutazama nyuma na kutambua umbali waliotoka pamoja.
Pia, walifunzwa namna ya kushughulikia migogoro kwa busara, kusikiliza mitazamo ya kila mmoja na kuepuka kuruhusu watu wa nje kuingilia masuala ya ndoa.