Pambo

Huu hapa misingi ya penzi la kudumu

Na BENSON MATHEKA April 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAPENZI ya kudumu hayajengwi kwa hisia pekee; yanahitaji bidii, kujitolea, mawasiliano ya wazi, na kuheshimiana.

Katika dunia ya sasa ambapo mahusiano mengi huvunjika kwa sababu ya kutoelewana, usaliti na mawasiliano duni, wanasaikolojia wanasema ni muhimu kujifunza misingi inayosimika mapenzi ya kudumu.

Kwanza kabisa, ili upendwe na kukumbatiwa ni muhimu kuwa msafi na kupendeza. Harufu nzuri na usafi wa mwili, ukiongeza manukato, huvutia wapenzi kwa njia ya kipekee.

Tenga muda na rasilimali kujiweka safi – piga mswaki asubuhi na jioni, oga kila siku au hata mara mbili kwa siku, nenda saluni utengeneze nywele ziwe maridadi, pitia kinyozi kila wiki kidevu kichongwe sawa, tengeneza kucha ziwe safi na laini usiache ziwe chafu na chwara kama vijembe.

Pili, uaminifu hukoleza mwenzio anapokuwa na unahika kwamba anaweza kukuamini. “Unahitaji kuwa mtu wa kuweka siri na mambo ya faragha, epuka kuhukumu kila kosa, kuwa na msimamo, na mtu mwenye utu,” asema mwanasaikolojia Janet Kane.

Ikiwa unataka mwenzi wako awe na shauku nawe kimapenzi, jiheshimu na udumishe mvuto wa mwili na kiakili. “Mapenzi si jambo la kubahatisha; ni kazi ya kila siku. Urembo wa ndani una nafasi kubwa zaidi kuliko kuwa na sura nzuri pekee,” aeleza Kane.

Anasisitiza kuwa uhusiano wowote wa kudumu unahitaji mawasiliano. “ Unapotaka kusikilizwa, ongea kwa uwazi na kwa heshima. Vile vile, ukitaka mpenzi wako akujali, jifunze kumsikiliza kwa makini na kuomba msamaha kwa unyenyekevu na moyo wa toba,” asema mwanasaikolojia huyo.

Ikiwa unataka mpenzi wako awe akikuwaza kila mara mfanyie mambo spesheli – madogo au makubwa, ya kawaida au mapya – yatakayosalia daima moyoni mwake. Funguka ili akujue kwa undani, si juu juu tu. Jionyeshe kuwa mtu wa thamani, mwenye maono, msimamo na heshima.

Mapenzi ya kudumu na yenye baraka huanzia kwa Mungu. Ikiwa unataka uhusiano thabiti mfuate Mungu na uchague mwenzi ambaye pia anamcha Mungu.Uwajibikaji huleta uhuru wa kweli, na kusema ukweli hujenga uaminifu.

Tabia njema ni ya thamani zaidi ya mali, huu ni msingi na kiitikio cha mapenzi ya kudumu. Kulingana na Kane, ikiwa unataka mtu awe nguzo yako maishani, usiogope kuonyesha udhaifu wako.

Uhusiano wa kudumu hujengwa kwa kusaidiana, na huwezi kusaidia mtu iwapo hujui anahitaji msaada wa aina gani.“Shiriki ndoto zako, mipango yako na changamoto zako ili mwenzio afahamu ni vipi atakufaa katika safari hii ya maisha. Mpe mwenzio nafasi ya kweli maishani mwako, si kwa maneno tu bali kwa vitendo,” Kane aongeza.

Ukitaka upendo wa kweli na wa kudumu, jifunze kuwa mtu wa kweli. Epuka maigizo na mzaha katika mapenzi.Vile vile, uwe mtu wa kukubali kujifunza na kurekebishwa kwani uhusiano mzuri ni ule unaotoa fursa ya mabadiliko kwa wema.

Mwisho, uwe mtu aliye tayari kutetea na kulinda mpenzi wake. “Ikiwa kweli unatamani mapenzi ya kudumu, chagua kupenda kila siku. Si siku za raha tu, bali hata zile ngumu. Mapenzi yanapimwa zaidi nyakati za majaribio kuliko raha,” ahitimisha [email protected]