Pambo

Jifunze lugha ya mapenzi ya mtu wako kunogesha ndoa

Na  BENSON MATHEKA September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katika jamii nyingi za Kiafrika, mada ya ngono bado ni mwiko, hasa inapozungumzwa hadharani au ndani ya nyumba za ibada.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa masuala ya ndoa na familia wanaamini kuwa iwapo makanisa na wahubiri wangekuwa wazi zaidi kuhusu masuala ya ngono katika ndoa, kiwango cha talaka kingepungua kwa kiasi kikubwa hata kufikia chini ya asilimia 50.

Wanasema kwamba ukweli mchungu ni kuwa matatizo mengi ya ndoa yanahusiana kwa njia moja au nyingine na kutotimizwa kwa mahitaji ya ngono.

Matatizo kama hasira, kutoelewana, kuchukiana, kulipizana kisasi, au hata kutoka nje ya ndoa huweza kuchochewa na hali ya kutoridhika kwa mtu na tendo la ndoa.

Mwanasaikolojia Sam Olade anasisitiza kuwa ngono ni zaidi ya kuungana kimwili. Ni tendo linalohitaji maandalizi ya kihisia, kimapenzi na kimwili – hasa kwa wanawake. Kwa hivyo, wanaume wanahimizwa kuelewa saikolojia ya wake zao na kuwalisha hisia na mapenzi hata kabla ya tendo lenyewe.

“Usimchukulie mkeo kama mashine ya ngono, mheshimu, mpe mapenzi na mjali kama mpenzi wako wa kweli,” asema Olade

Anaongeza: “Matamshi ya kimahaba ni muhimu, wanawake huvutiwa na maneno ya mapenzi. Mwambie  “nakupenda”, “wewe ni mrembo”, “nashukuru kuwa na wewe”  mara kwa mara si wakati wa tendo pekee.

Mguso wa kimapenzi wa kila siku, asema, kama vile kumkumbatia, kumshika mkono, kumbusu bila sababu, kumchezea chezea huongeza ukaribu.

“Jifunze lugha ya mapenzi ya mkeo. Kila mtu ana njia yake ya kujihisi kupendwa. Inaweza kuwa kwa maneno, zawadi, muda wa pamoja, kuguswa au kusaidiwa kazi.Usikimbilie tendo. Wanaume wanashauriwa kutumia muda wa kutosha kumwandaa mke wao kihisia na kimwili kabla ya tendo la ndoa,” asema Olade

Wataalamu wa masuala na ndoa wanasema tendo la ndoa huridhisha  pale  wenzi wa ndoa wanapoheshimiana na wanapoonyeshana mapenzi. Burudani hili huwa ya kuridhisha na ndoa huimarika.

Olade anakumbusha kwamba ngono ni zawadi ya Mungu kwa wanandoa, na ni jambo la faragha na heshima.

Wanaume na wake wanapaswa kujifunza na kuboresha maisha yao ya ndoa kwa njia ya mawasiliano ya wazi baina yao, heshima na mapenzi na sio kuanika faragha yao kwa watu wengine.

“Ngono bora ndani ya ndoa huleta mshikamano, furaha na upendo wa kweli. Wenzi wanaoridhishana kimapenzi huwa na ndoa thabiti na yenye furaha,” asema.