Jinsi ya kukabiliana na upweke katika ndoa
WIKI iliyopita tulichambua chanzo cha upweke katika ndoa.
Tulijifunza kuwa chanzo kikuu cha upweke katika ndoa na wanadoa kukosa mawasiliano.
Leo, tunaendelea na mjadala huu muhimu, safari hii tukiangazia jinsi ya kukabiliana na upweke ili kuijenga upya mahusiano yenu.
Bi Elizabeth Magotsi, mhubiri na mshauri wa masuala ya ndoa anatueleza kuwa wanadoa wanaweza kukabiliana na upweke kwa njia zifuatavyo:
Kuwa na mazungumzo ya ndani
Katika safari ya ndoa, mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya ukaribu. Bila mawasiliano, wanandoa huanza ‘kutengana’ kihisia pole pole.
“Wanandoa wanapaswa kuzungumza kwa uwazi, bila hofu ya kuhukumiwa. Mazungumzo yaweza kuwa madogo, lakini athari yake ni kubwa sana,” anasema Magotsi.
Kando na hayo anasema kuwa kuna umuhimu wa kujenga mazoea ya kuzungumza si tu kuhusu majukumu ya kila siku, bali kuhusu hisia, ndoto, matarajio na hata mambo madogo yanayoleta furaha au wasiwasi.
Tengeni muda wa kushiriki pamoja (mke na mume)
Majukumu ya kazi na familia mara nyingi hutenganisha wanandoa. Lakini Bi Magotsi anasisitiza umuhimu wa kupanga muda mahsusi wa kuwa pamoja – iwe ni date night, kutembea jioni, au dakika chache za kahawa mkiwa wawili bila kelele za watoto.
“Muda huu unaweza kunekana kuwa mdogo lakini unaweza kufufua mapenzi na kufanya ndoa iwe imara.”
Uwe na moyo wa shukrani
Kila mmoja anapenda kuthaminiwa. Ukiona mwenzako ametengeneza kitanda, ameandaa chakula au anamlea mtoto ukiwa umechoka, sema asante. Hii ina uwezo wa kuimarisha mahusiano.
Hisia ya kutambuliwa huondoa upweke na kujenga mazingira ya upendo.
Punguza muda wa kutumia simu
Teknolojia ni baraka na wakati mwingine laana kwa ndoa. Simu inapokuwa rafiki wa karibu kuliko mwenzako, upweke hutawala.
“Wakati mwingine, wanadoa wanafaa kuweka sheria kama vile kutenga muda fulani wa kutumia simu. Baada ya muda huo kukamilika, mnafaa kutumia nafasi hiyo kuzungumza, kucheka, na kujenga urafiki wa kweli ndani ya ndoa,” anaongeza Bi Magotsi.
Tibu vidonda vya zamani
Wengi hubeba maumivu ya zamani moyoni; maneno mabaya, kutokuaminiana, au matendo yaliyowaumiza. Vidonda visipotibiwa, mtu hujifunga na kujitenga.
“Msione haya kuzungumza kuhusu yaliyowaumiza. Sameheaneni na muanze upya,” anashauri Bi Magotsi.
Tafuteni ushauri wa kitaalamu
Kuna wakati mazungumzo ya kawaida hayatoshi. Hapo ndipo kuna haja ya kumwona mshauri wa ndoa. Mshauri husaidia wanandoa kuelewa tabia zao, mitazamo yao, na jinsi ya kujenga mawasiliano bora.