Pambo

Jinsi ya kutuliza janadume

Na BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IKIWA unataka mume wako atulie nyumbani changamka na umpe shibe yake ya mahaba kila anapotamani.

Ngono ina uwezo wa kiajabu kumtuliza mwanamume. Utabadilisha hisia zake kwa dakika chache tu hasa ikiwa ni wewe uliyewasha moto huo wa huba.

Lakini ikiwa nyumbani ni mabishano na ugomvi mwingi, kumlipukia kila mara na kumfanya akose utulivu, atahofia kurudi na kuanza kutafuta pahali pa kukimbilia.

Wanawake wanaowajulia waume wao hujua jinsi ya kumteka akili na hisia, kumfanya atulie nyumbani.Mpe anachopenda kufanya ili afurahie kuwa nawe, naye ataganda kwako kamwe hatobanduka.

“Wanaume huwa na vitu wanavyopenda ili wafurahi. Yaweza kuwa shughuli fulani au mahali; labda ni chumba cha michezo, kutazama runinga, kutafakari, kuandika, kusoma, kuimba, kufanya mazoezi au kupumzika. Usivuruge eneo hili au shughuli zake, bali kubaliana naye jinsi ya kusawazisha vyema muda wake ili asitumie mwingi sana huko,” aeleza mtaalamu wa mahusiano Caleb Mutinda.

Anahoji kuwa wanaume wanakumbwa na msongo wa mawazo kwa sababu za kifedha na wadada wanaotambua hili na kuwasaidia huwafanya watulie.

“Mpunguzie presha ya maisha kwa kulipa baadhi ya bili, mfae kwa mbinu mwafaka za kutunza fedha vyema zaidi, utafuta mradi wa kuwekeza kwa muda mrefu, na kushika hatamu za kugharamia mahitaji ya nyumbani hasa wakati amepoteza kazi au amepata hasara katika biashara. Fanya haya kwa heshima wala usiingie kiburi na dharau. Kwa njia hii utamletea utulivu na kumweka kwapani,” aeleza Mutinda.

Wanawake wanaotambua waume zao huchoka na kupitia msongo wa mawazo, na kuwasaidia kipindi hiki huwa wanawapa motisha ya kunyanyuka na kushughulikia familia zao kila siku kwa nguvu mpya.

“Mkumbushe ukuu wake, sherehekea mafanikio yake na umwambie jinsi unajivunia kuwa naye. Hii inampa motisha,” asema Ivy Wawira, mjuzi wa mahusiano ya mapenzi na mshauri wa ndoa.Zaidi ya yote, asema Wawira, majanadume yanapenda mwanamke mwaminifu.

“Hakuna kitu kinachovuruga mwanamume kama kuhisi au kugundua mke wake, ambaye anampenda na amempa kila kitu, anapepesa macho kwa jamaa mwingine. Ukiepushia mumeo mateso haya ataganda kwako,” anasititiza.

Wanaume huonyesha uso mgumu na hujibania mambo kwa sababu hawaamini tu mtu yeyote. Hii ndiyo sababu wengi wao huathiriwa na msongo wa mawazo na kuteseka kimyakimya.

“Wanatamani kupata mtu wa kuamini, wa kuwafungulia roho wajue hisia zao za ndani, wawaonyeshe furaha yao na pia maumivu ya moyoni. Kama mkewe kuwa mtu huyo kwake,’” aeleza Wawira.

Dekeza mtu wako, mpe busu sio tu mdomoni, hata mashavu, mikono na mgongoni huku ukimporomoshea maneno kwamba unampenda. Pia fanyeni kitu kipya pamoja kwani utamfanya ajisikie upya na kukufikiria zaidi unapokuwa mbali naye.