Kaka, chunga usipoteze nafasi ya kuwahi demu mpoa
Katika dunia ya leo ambayo imejaa mapenzi ya kuiga, tamaa, na mahusiano ya kimaslahi, kumpata demu anayependa kwa dhati ni baraka ya kweli kutoka kwa Mungu.
Mwanadada wa aina hii haangalii tu kile ulichonacho, balianakupenda kwa jinsi ulivyo pamoja na mapungufu yako, ndoto zako, na hata maumivu yako. Ni demu anayekubali kutembea nawe katika giza, si kwa sababu ya nuru yako, bali kwa sababu anaamini kwa kilicho ndani yako hata kabla hakijaangaza au hata hakuna ulicho nacho.
“Demu anayependa kwa dhati ni nguzo ya maisha ya mwanaume,” asema Mercy Kiio, mtaalamu wa ndoa na mahusiano. “Anakuwa bega la kulilia, moyo wa kufariji, na mshauri wa kutegemea. Hatapenda kwa maneno matupu bali kwa vitendo na heshima. Atakuunga na kukuhimiza unapojaribu, atakuinua unapovunjika moyo, na atakukumbusha thamani yako unapojisahau. Yeye si tu mpenzi, bali rafiki wa kweli, mshirika wa kiroho na nguzo ya kimapenzi yenye msingi wa heshima na maombi,” asema Mercy.
Kulingana naye, japo chochote king’aacho si dhahabu, mapenzi ya dhati ya manzi hayajifichi. “Yanaonekana kwenye jicho lake, kwenye matendo yake ya kila siku, kwenye sala anazokuombea usiku, na kwenye uvumilivu wake anapokabiliana na hasira zako, ukimya wako au ugumu wa maisha. Mwanadada wa namna hii hataki mengi, ila anatamani kujua kwamba anathaminiwa, anapendwa na yuko salama katika moyo wako,” aeleza.
Wataalamu wa mahusiano wanasema ni ni kosa kubwa kumchukulia mwanadada anayependa kwa dhati kama jambo la kawaida. Wanaume wengi wamepoteza wanawake wa aina hii kwa sababu ya kutokuwa waaminifu, kutojali, au kuruhusu majaribu ya nje kuharibu penzi halisi. Mwanadada anayependa kwa dhati akiumia sana, anaweza kuondoka kimya kimya na ndipo mwanaume huanza kuona pengo la upendo wake wa kweli,” asema Lenny Mwaniki, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya mahusiano.
Wanaume wengi, asema, huja kutambua thamani ya demu mzuri baada ya kumpoteza. “Wanaangalia nyuma na kutamani warudishe muda nyuma, lakini wanakuta mwanamke huyo amejifunza kujipenda na kujisamehe kwa kumpenda mtu asiyeweza kuthamini upendo wake.”
“Mtunze mwanamke wa aina hii ukibahatika kumpata. Mthamini kwa matendo, maneno, na uaminifu. Mpe nafasi ya kushamiri katika maisha yako. Sema asante kwake, mweleze unampenda, na msikilize kwa moyo safi. Hakikisha moyo wake hauna shaka nawe, bali uwe na uhakika kwamba moyo wake umejaa amani kwa sababu anajua unathamini upendo wake,” ashauri Mercy.
Mwaniki anaongeza: “Mwanadada anayependa kwa dhati si tu mwenzi wa maisha ni baraka, ni zawadi, ni mshirika wa milele. Usimpoteze, mtunze, mthamini. Ni johari nadra katika ulimwengu wa sasa.”