Kukabili ukatili miongoni mwa watoto
UKATILI wa wanafunzi kwa wenzao unaweza kutokea mahali popote, na kwa mtoto yeyote. Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti mpya, baadhi ya watoto wako katika hatari kubwa zaidi ya kudhulumiwa kuliko wengine.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nebraska, mjini Lincoln, waligundua kuwa wanafunzi wanaopokea huduma za elimu maalum kwa matatizo ya tabia, pamoja na wale walio na ulemavu unaoonekana wazi (kama matatizo ya lugha au kusikia), wana uwezekano mkubwa wa kuwa waathiriwa wa ukatili wa wanafunzi wenzao kuliko wale wa elimu ya kawaida.
Zaidi ya hayo, watoto hawa pia wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwadhulumu wenzao.Utafiti uliochapishwa katika Journal of School Psychology ulifuatilia zaidi ya wanafunzi 800 wa elimu maalum na ya kawaida, wenye umri wa kati ya miaka tisa hadi 16, katika shule tisa za msingi, kati na upili.
Matokeo yalionyesha kuwa watoto wanaopokea elimu maalum walikuwa na uwezekano mkubwa si tu wa kudhulumiwa, bali pia wa kuwadhulumu wengine.
Asilimia 67 ya wanafunzi hao waliripoti kuwa wamewahi kudhulumiwa, huku zaidi ya theluthi moja (asilimia 38.1) wakikiri kuwa wamewahi kuwadhulumu wanafunzi wenzao.
Waandishi wa utafiti huo wanaeleza kuwa watoto wenye ulemavu unaoonekana wanaweza kuwa waathiriwa wa ukatili kwa sababu huonekana kuwa rahisi kudhulumiwa. Pia wanapendekeza kuwa baadhi ya watoto hao wanaweza kujihusisha na ukatili kama njia ya kulipiza kisasi.
Kwa mujibu wa matokeo, wanafunzi wa elimu maalum pia walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupelekwa ofisini kwa mwalimu mkuu kwa sababu ya masuala ya nidhamu.
Utafiti pia ulibaini kuwa tabia ya ukatili sio kwa jinsia moja pekee. Wasichana na wavulana wote walionekana kuathiriwa kwa kiwango sawa.
“Tumesoma habari za kusikitisha kuhusu watoto na vijana waliokatiza maisha yao baada ya kukumbwa na ukatili wa mara kwa mara na wa kudumu. Mbali na vifo hivyo vya kuhuzunisha, kuna athari nyingine nyingi za ukatili ambazo huenda haziripotiwi mara kwa mara lakini ni muhimu sana kushughulikiwa,” asema mtafiti na mtaalamu wa malezi Dkt Debbie Glasser.
Anatoa mfano wa watoto wanaodhulumiwa akisema wanaweza kuanza kukumbwa na wasiwasi, huzuni, na matatizo ya kiafya.Wazazi, walimu na wataalamu wengine wanapaswa kufahamu viashiria vya hatari na dalili za ukatili.
Baadhi ya ishara kwamba mtoto anaweza kuwa anadhulumiwa ni:Kukosa usingizi au kuwa na ndoto mbaya mara kwa mara, mabadiliko ya tabia ya kula, kutafuta visingizio vya kuepuka kwenda shule, majeraha yasiyoelezeka, kupoteza au kuharibu vitu vya thamani (kama pesa, iPad, simu), kupungua kwa hali ya kujiamini, kuongezeka kwa malalamishi ya maumivu ya kichwa au tumbo na kushuka kwa ghafla kwa alama za mitihani.
Hata hivyo, kuwepo kwa tabia hizi hakumaanishi moja kwa moja kwamba mtoto anadhulumiwa. Ikiwa mzazi au mlezi ana wasiwasi kuhusu mtoto wake, anapaswa kutafuta msaada kutoka kwa mtaalamu.
Watafiti wanatoa mapendekezo kadhaa kulingana na matokeo yao. Wanashauri kuwa mipango ya kuzuia ukatili inapaswa kutekelezwa kwa wanafunzi wote wa elimu maalum na ya kawaida, ili kukuza ujuzi wa kijamii.
Wanatumai kuwa wanafunzi wenye ujuzi wa kijamii wanaweza kuwa mfano mwema kwa wenzao.Pia, wanapendekeza kuwa walimu na wafanyakazi wa shule wawasaidie wanafunzi wenye ulemavu unaoonekana katika madarasa ya elimu ya kawaida ili kusaidia kupunguza visa vya ukatili.