Pambo

Kukidhi mahitaji ya ndoa si hisani wala tafadhali

Na BENSON MATHEKA December 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANANDOA huapa kulindana kwa hali na mali hadi kifo kiwatenganishe.

Hakuna kiapo cha ndoa kisichokuwa na maneno hayo. Ahadi nyingine ni kwamba wawili wameungana kuwa kitu kimoja. Hii inamaanisha kila mmoja, mume na mke, anafaa kumchukulia mwenzake kama sehemu yake na kusaidiana katika kila hali.

Kusaidiana huku ni kutekeleza majukumu ya ndoa kwa ushirikiano – hakuna jambo ambalo mume au mke anatengewa kutimiza peke yake.Wengi hukariri kiapo hiki, hususan wanawake wanapotaka waume wao kuwajibikia pia kazi za nyumbani.Ni sawa kabisa kutaka mwenzio ajukumike kwa hilo kwani ni sehemu ya kusaidiana katika kila hali.

Hata hivyo, mume kukusaidia kusonga ugali jikoni au kufua nguo hakubadilishi nafasi yake kama kiongozi wa familia. Kuna wanawake wanaoamini kuwa faida ya mume ni wakati ana uwezo wa kukidhi mahitaji ya familia.Kwa dhana hiyo potofu wengi wameishia kuwaacha waume zao wanapopungukiwa kifedha.

Katika karne hii inayokumbatia usawa wa jinsia, wanawake wanafaa kubadili mawazo na kukubali jukumu la kukidhi mahitaji ya familia mzima mzima, au kulichangamkia iwapo mume ameghafilika kwa njia moja au nyingine.

Kasumba ya baadhi yao kwamba hawawezi kulisha mwanamume mwenye kidevu ambaye si kakake wa kuzaliwa, imekolea kutokana na itikadi za kale zilizokumbatiwa na mababu wetu ambao hawakuwa wameelimika.

“Kukidhi mahitaji ya familia si kibali kwa mwanamke kumbeza mumewe. Kwake kutekeleza wajibu huo si hisani kwa mume bali ni jukumu la ndoa ambalo aliapa kutimiza alipokula kiapo,” anatanguliza mshauri wa masuala ya ndoa Saida Wanjiru.“Wanawake wamekuwa wakipigania usawa wa jinsia. Hivyo, hawawezi kukwepa kuwajibika kikamilifu katika jukumu lolote la ndoa,” anaongeza.

Saida anatoa mfano wa wanawake wengi tu wasio na waume lakini familia zao zinanawiri, na hivyo kubomoa dhana kwamba mwanamke hawezi au hafai kuendesha familia.Kuna wanawake waliobahatika kupata mali au kusoma kuliko, kwa mfano, kaka zao wanaosimamia shughuli za familia wanakotoka.

“Je, mwanamke akifanikiwa kuliko mumewe aache familia yake iyumbeyumbe katika umaskini kwa sababu tu ya taasubi kwamba mume ndiye wa kushughulikia mahitaji yote?” auliza mshauri Saida.Kwa upande mwingine, wanaume wanaozuia wake zao “kukohoa” katika familia wanaishi karne za mababu, na itawalazimu kukumbatia uhalisia wa maisha ya kizazi cha sasa.

“Yote tisa, nasisitiza kwamba mke akijaliwa ukwasi wa fedha hafai kudharau mumewe. Mume naye aheshimu mke anapoamua kuchangamkia jukumu la kukidhi mahitaji ya familia, na kumpa sapoti kwa kumsaidia katika kazi zingine.

Ndoa ni kushauriana na kusaidiana; nguzo hii isiwe tu maneno tupu na kutiwa katika kaburi la sahau baada ya kula kiapo cha ndoa,”asema. [email protected]