Pambo

Mabibi waingiwa na wasiwasi waume wakienda kunyolewa

January 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

KWA kawaida, huwa haimchukui mtu muda mrefu kunyolewa katika duka la kinyozi.

Ikizingatiwa kuwa huwa kuna wateja wengi katika maduka hayo, baadhi ya wahudumu wa vinyozi huwanyoa wateja wao kwa haraka ili kumhudumia kila mmoja aliyefika kwa ajili ya kunyolewa.

Hata hivyo, hali imeonekana kubadilika, hasa katika maeneo ya mijini, kwani vinyozi sasa vimegeuka kuwa sumaku kwa wanaume.

Ingawa mtu huenda kunyolewa baada ya nywele yake kumea—pengine baada ya majuma matatu au hata mwezi mmoja—hali hiyo inaonekana kubadilika—hasa kutokana na mchipuko wa vinyozi vya kisasa.

Vinyozi hivyo vina upekee wake.

Kando na uwepo wa wahudumu wa kawaida ambao huwanyoa watu, sasa kumeibuka mtindo mpya, ambapo kuna wanadada ambao huwanyoa wanaume, kuwapakata na hata kuwachezea densi.

Hayo ndiyo mazingira mapya kwa mwanadada Mwende Frey.

Katika duka lake la kinyozi la Manchambers lililo katika eneo la Kamakis, By-Pass, Kaunti ya Kiambu, huwa kuna ujumbe ulioandikwa kwa herufi kubwa: Hiki ni kinyozi cha wanaume pekee.

Je, sababu ya tahadhari hiyo ni ipi?

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mwanadada huyo anasema hilo linatokana na huduma ambazo huwa wanawapa wateja wao.

“Hiki ni kinyozi cha kipekee. Wafanyakazi wangu huwa ni wanadada pekee. Sababu ya hili ni kuondoa dhana kwamba taaluma ya kuwanyoa watu inaweza tu kufanywa na wanaume,” akasema Bi Mwende.

Kwenye duka hilo la kinyozi, mteja huwa ananyolewa vizuri na mwanadada aliyevalia nadhifu.

Baadaye, huwa anapakatwa na kukandwa, yaani kufanyiwa massage, huku akichezewa densi na mwanadada mwingine.

“Wengi wamekuwa wakifasiri vibaya huduma tunazotoa. Hata hivyo, ukweli ni kuwa hii ni njia mojawapo ya kuwaburudisha wateja wetu,” akasema Bi Mwende.

Anasema kuwa mbinu hiyo imekuwa ikiwavutia wateja wake, kwani kando na kunyolewa, wao huhisi “makaribisho mazuri kwa huduma kama kupakatwa na kukandwa”.

“Wateja wetu wengi ni watu wanaotoka kazini. Hivyo, wengi huwa wamechoka. Hii ni njia moja ya kuwaburudisha, kuwaondolea uchovu na mawazo ambayo huenda wakawa nayo,” akasema Bi Mwende.

Anasema kuwa kwa kutumia mbinu hiyo, wanaume wengi wamekuwa wakifika kutafuta huduma hizo baada hata mara mbili kwa wiki.

Mteja mmoja, aliyejitambua tu kama Lawrence, alisema kwamba vinyozi kama hivyo vimekuwa vikimvutia sana, kwani huwa kama “kitulizo kwangu”.

“Baada ya kazi, mara kwa mara huwa napita hapo, kwani baada ya kukandwa, huwa ninajihisi kama mtoto mdogo. Mawazo niliyo nayo huwa yamenipungukia kabisa,” akasema.

Wateja wengi waliozungumza nasi walisema kwamba raia wanafaa kuondoa dhana mbaya walizo nazo kuhusu vinyozi hivyo.

Aidha, wanaume walisema mabibi–wake– wao hawafai kuwa na wasiwasi wao kuhudumiwa na wanawake kwa sababu hakuna la zaidi linaloendelea pale.