Pambo

Makosa madogo yanayoharibu ndoa

May 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA NENSON MATHEKA

HAKUNA anayeingia katika ndoa akiwa na nia ya kuiharibu.

Hata hivyo, ni rahisi kuharibu ndoa kuliko kuijenga. Ndoa inaweza kuharibiwa na makosa madogo yanayoweza kuepukika hasa yanapopuuzwa.

“Ikiwa unataka kuharibu ndoa yako, puuza Mungu nyumbani kwako, usimpe nafasi hata kidogo, weka Mungu kando na uthamini anasa, dhambi na udhalimu,” asema mshauri wa ndoa Doreen Kerubo ambaye pia ni mwanasaikolojia.

Watu wanaingia katika ndoa wakiwa na matumaini ya maisha yenye furaha lakini kwa sababu ya kupuuza maisha yao ya kiroho wanaisambaratisha.

“Raha inapaswa kuwa kiasi, na katika kuwania hiyo raha, usimtenge mtu wako,” asema Kerubo.

Makosa ya watu walio katika ndoa, ni kutumia muda wanaopaswa kuwa na wachumba wao kwa mambo mengine ya kibinafsi.

“Ukitaka kuharibu ndoa yako, kamwe usitumie muda na mume au mkeo. Shinda ukiwa na marafiki zako katika chama, wafanyakazi wenzako na safari za kazi. Ukifanya hivi utapata hautakuwa na ndoa na utajilaumu mwenyewe,” aeleza Kerubo.

Mume au mke ni mtu spesheli katika maisha yako na haufai kumchukulia kama mtu kwa kawaida. Haufai kumchukulia kama watu wengine.

“Watu huwa wanaharibu ndoa zao kwa kuwachukulia waume na wake zao kama watu wa kawaida, wanakosa kuwajali na kuwaheshimu. Unapata mtu akiita mume au mke wake majina ya kumdhalilisha. Usipothamini mume au mkeo kama mtu spesheli kwa maisha yako unaharibu ndoa yako,” aeleza Kerubo.

Kulingana na mwanasaikolojia James Kariuki, watu huwa wanaharibu ndoa zao kwa kuwapa presha waume au wake zao. Unapata mtu anapenda kulalamika bila kikomo kwa chochote ambacho mume au mke anafanya.

RAHA YA NDOA

“Ukitaka ndoa yako ikose raha na kuvunjika haraka, usimpe mtu wako nafasi ya kupumua. Mpe presha. Lalamika hata kwa mambo madogo,” aeleza Kariuki.

Japo kazi ni nzuri, wataalamu wanasema inaweza kuharibu ndoa hasa pale wanawake wanapoitumia kujitenga na waume zao.

“Mke, ukitaka kuharibu ndoa, zamia biashara na kazi yako na upuuze mume na watoto wako. Ukifanya hivi, ndoa haitadumu na hata mumeo akikuvumilia, atachepuka. Sawazisha muda wa kazi, familia na usikose kutenga muda wa kuwa na mumeo,” asema Kariuki.

Kerubo anaongeza kuwa hii ni kwa wanaume pia.

“Wanafaa kuhakikisha wanapata muda wa kuwa na wake zao hata wanapohakikisha vyanzo vyao vya riziki haviyumbi,” aeleza.

Watu huwa wanaharibu ndoa zao kwa kuzungumzia wapenzi wao wa zamani mara kwa mara wakiashiria kwamba walikuwa bora kuliko waume au wake zao.

Kerubo anasema watu huwa wanaharibu ndoa zao kwa kuwapimia waume au wake zao tendo la ndoa.

“Usinyime mtu wako tendo la ndoa na usimuumize ukidai haki yako ya tendo la ndoa. Timizianeni haki hii kwa upendo na kujali kila mmoja,” asema.