Malezi: SMS kwa wingi hupunguza ujuzi wa lugha
KUTUMA ujumbe mfupi huwapa watoto na watu wazima njia ya haraka na rahisi ya kuwasiliana, lakini kuna madhara ya kutumia njia hizi za mkato.
Kwa mujibu wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Penn State, Amerika mazoea ya kutumia jumbe fupi kwa mawasiliano miaka ile ya mwanzoni ya kuweka msingi wa masomo mwanafunzi akiwa shuleni, kunaweza kupunguza ujuzi wa lugha na sarufi.
Katika utafiti uliochapishwa kwenye jarida la New Media & Society, watafiti waliwapa wanafunzi wa shule za sekondari mtihani wa tathmini ya sarufi kulingana na dhana walizofundishwa wakati wa mwaka wa masomo.
Walikusanya taarifa kuhusu tabia za wanafunzi katika kutuma ujumbe mfupi, ikiwa ni pamoja na mara wanazotuma na kupokea jumbe. Pia, waliwauliza wanafunzi waandike idadi ya mafupisho (yaani, njia fupi za kuandika ujumbe) walizotumia katika jumbe zao tatu za mwisho.
Watafiti waligundua kuwa matumizi ya njia fupi za kuandika ujumbe yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mawasiliano rasmi. Katika utafiti huu, matumizi ya jumbe fupi kwa wingi yalihusiana na utendaji duni wa wanafunzi katika mtihani wa sarufi.
Katika ulimwengu wetu wa teknolojia ya kisasa, kutuma ujumbe na njia nyingine za mawasiliano ya haraka kutaendelea kuwepo. Hilo si jambo baya kabisa. Kutuma ujumbe huwapa watoto wetu njia rahisi na ya haraka ya kujieleza.
“Lengo letu kama wazazi si kujaribu kuondoa matumizi ya arafa kabisa! Badala yake, kuna mambo tunayoweza kufanya ili kusaidia kukuza ujuzi wa lugha na uandishi kwa watoto wetu wanapokua,” asema Dkt Debbie Glasser, mmoja wa watafiti hao.
Wataalamu wanashauri wazazi kuchukua muda kuwasiliana na watoto kwa sentensi kamili.“Unapowatumia watoto wako ujumbe, chukua muda wa ziada kuwasiliana kwa sentensi kamili mara kwa mara.
Kuna utafiti unaopendekeza kuwa watoto huwa na hamu ya kuiga marafiki na familia zao. Hii ni fursa nzuri kuwa mfano mzuri katika matumizi ya sarufi sahihi,” aeleza Dkt Debbie.